Tambwe atoa ya moyoni hapo Yanga

Muktasari:

Tambwe aliyejiunga na Yanga katika usajili wa dirisha dogo msimu wa 2014-2015

Dar es Salaam. Amissi Tambwe amesema yuko tayari kucheza klabu yoyote nchini licha ya kurejea Burundi, baada ya kuachwa na Yanga katika usajili wa msimu ujao.

Hata hivyo, alisema hataisahau Yanga katika maisha ya soka kwa kuwa ndio klabu iliyompa thamani baada ya kutemwa na Simba licha ya kutwaa tuzo ya mfungaji bora msimu 2013-2014.

Tambwe aliyejiunga na Yanga katika usajili wa dirisha dogo msimu wa 2014-2015, alisema baadhi ya klabu zimeweka ofa mezani ya kumsajili, lakini hajatia saini kwa kuwa yuko Burundi.

Tambwe alisema amerejea Burundi baada ya Yanga kutompa mkataba mpya, lakini atarejea kufuata fedha anazoidai klabu hiyo.

“Yanga hawana mpango wa kuniongeza mkataba nimeamua kuondoka, niko Burundi nikijipanga upya kuangalia maisha mengine ya soka nje ya Yanga,”alisema Tambwe.

Nyota huyo alisema katika kipindi alichokuwa nchini alifurahia maisha ndani na nje ya soka, hivyo atakuwa tayari kurejea kucheza soka kwa kuwa ni sehemu salama.

Akizungumzia Yanga, Tambwe alisema ni miongoni mwa klabu bora za Afrika na imekuwa sehemu ya mafanikio katika maisha yake ya soka na binafsi.