Taifa Stars yafanya kliniki kwa watoto, Samatta atoa neno

Wednesday November 13 2019
pic Stars

Dar es Salaam. Wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo wametembelea shule ya msingi Laureate International na kushiriki katika kliniki ya soka la vijana kuanzia miaka 5 mpaka 15, shule hapo.

Taifa Stars inayojianda na mchezo wa kusaka kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika Cameroon 2021, ambao Ijumaa saa 1:00 usiku watacheza dhidi ya Equatorial Guinea kwenye Uwanja wa Taifa.

Akizungumza na wanafunzi hao nahodha Taifa Stars, Mbwana Samatta alisema wakati wao wanaanza kucheza soka kulikuwa hakuna walimu waliokuwa na uweledi wa mchezo huo tofauti na ilivyokuwa kwa watoto wa sasa.

“Hii ni fursa kubwa kupata waalimu wa kuwafundisha tangu mkiwa wadogo ni wajibu wenu kujituma zaidi.”

Katika hatua nyingine Samatta alisema maandalizi yao yanakwenda vizuri wamejipanga kutokufanya makosa kama ambayo waliyafanya huko nyuma.

"Ukiangalia timu yetu inatafuta nafasi ya kwenda kupata uzoefu wa kushiriki na si kutwaa ubingwa kwani tulikuwa nje ya mashindano haya zaidi ya miaka 30, kwa maana hiyo tunatakiwa kupata nafasi ya kwenda kushiriki zaidi ya mara tano tena mfululizo," alisema.

Advertisement

"Kuna timu za taifa zinakuja katika mashindano ya Afcon bajeti zao ni kubwa kuliko yetu, ina wachezaji wanaocheza mashindano hayo mara kwa mara, lakini wanatoka katika ligi bora tena zenye ushindani mkubwa, ingawa katika soka lolote linaweza kutokea.

"Kwangu naamini tutaweza kucheza mashindano haya mara kwa mara tunaweza kuchukua ubingwa katika siku za usoni, lakini kwa wakati huu timu yetu ilivyo inafanya maandalizi ya kupata nafasi ya kushiriki jambo ambalo linawezekana," alisema Samatta.

Kocha wa Stars, Mrundi Ettiene Ndayiragije alisema kila mchezaji aliyemuita katika timu hiyo amekuja akiwa tayari kwa kushindana.

"Ukiangalia wapinzani wetu Equatorial Guinea, ina wachezaji wengi ambao si raia wa kuzaliwa wa nchi hiyo na katika kikosi chao cha kwanza kinawachezaji saba ambao wametokea Mbrazili na nchi nyingine kubwa," alisema.

"Nimepata muda wa kuangalia kanda zao za video nikiwa na wachezaji wangu ili kufahamu mbinu zao kwa maana ya ubora wao ili kuweza kuwazuia na madhaifu yao ili kuweza kuwashambulia, kuhusu kukosekana kwa Jonas Mkude hilo linaweza kuwa pengo kwani ni mchezaji muhimu ndio maana aliitwa.

"Nimejaribu kuita katika kila nafasi moja wachezaji wawili ambao wanaweza kucheza hapo kwa maana hiyo kutokuwepo kwa Mkude kuna ambaye atapata nafasi anatakwenda kuziba penge hilo," alisema Ndayitagije.

Advertisement