Taifa Stars vs Burundi katika lugha nyepesi zaidi

Tuesday October 13 2020

 

TULICHEZA dhidi ya Burundi juzi jioni pale katika ‘uwanja mbovu’ wa Taifa jijini Dar es salaam. Warundi waliichapa Taifa Stars bao 1-0 katika dakika za jioni. Dakika ambazo miezi ya karibuni tumezowea kumuona mlinzi Lamine Moro akiifungia timu yake ya Yanga mabao ya ushindi. Kulikuwa na matukio kadhaa ambao yalipita katika jicho langu. Yafuatayo yanaweza kuwa matukio ambayo niliyatazama kwa jicho tofauti kidogo na nikayaweka katika hisia zangu.

Samatta vs Martin Sanya

Sijui kulikuwa na nini katika kichwa cha Martin Sanya. Labda ndio maana miaka ya karibuni hatutoi waamuzi wazuri tofauti na zamani. Sanya alimpa kadi ya njano Samatta kwa kulalamika, alimsukuma wakati alipomfuata, alimtolea maneno makali ambayo hayaandikiki. Hii ni kwa mujibu wa Samatta. Hakuna kitu kibaya katika soka kama mwamuzi anapochezesha mpira akiwa na hisia za kujidharau na kutaka kujimwambafai (inferiority complex). Inaonekana Sanya aliingia uwanjani akiwa na hisia za ‘mimi simuogopi Samatta’... ‘atanikoma kwani yeye nani?’ Ilionekana wakati Samatta alipomlalamikia wakati akihisi kwamba haki ipo kwake. Waamuzi wa nje wamefundishwa saikolojia. Wanajua namna ya kumdhibiti mchezaji ambaye joto la mchezo limempanda. Wakati mwingine wanachofanya ni kutabasamu huku wakiendelea kutoa haki. Wakati mwingine wanaweza kukupa kadi ya njano huku wakicheka. Wanaamini katika sheria za mchezo na wanaamini katika uamuzi wao. Huku kwetu waamuzi kama Sanya wanadhani kuwakasirikia mastaa (kumbuka ni katika mechi ya kirafiki) kutawapa heshima. Unaitia mchezo ugumu usio na sababu. Samatta tunayemfahamu ana nidhamu ndani na nje ya uwanja. Kuna haja gani kujifanya mwalimu wa nidhamu kwa mchezaji nyota zaidi nchini ambaye amecheza mechi nyingi za kimataifa Ulaya kuliko hata ambazo Sanya amechezesha nchini?

Hatuna Chama wala Mukoko

Kuna mashabiki wakamlaumu kocha wa timu ya taifa ya Taifa, Ettiene Ndayiragije kwa kipigo cha juzi. Wakati mwingine tujiulize. Angefanya nini zaidi? Stars walicheza vyema katika kipindi cha kwanza. Nilipenda mbinyo walioutoa kwa wachezaji wa Burundi ambao nao sio wabaya. Ni mastaa wakubwa. Ungeweza kuona Taifa Stars wakipanga mashambulizi kuanzia mbele mpaka nyuma. Katikati Jonas Mkude alikuwa akicheza vyema, Fei Toto alikuwa akicheza vyema, na hata Said Ndemla alikuwa akicheza vyema. Tatizo letu kubwa ni eneo la mbele. Hakukuwa na shuti hata moja lililolenga lango hadi wakati tunakwenda mapumziko. Kuna mambo mawili hapa. Kwanza tuna ugonjwa wa kukosa kiungo mshambuliaji ambaye ni mbunifu kutengeneza nafasi au kufunga. Natamani tungekuwa na mchezaji wa aina ya Clatous Chotta Chama. Kina Fey ni wazuri kutawala dimba, lakini siamini kama wana ubunifu mkubwa eneo la mwisho kama kina Chama. Lakini pia kama washambuliaji hawachukui nafasi zao basi tunahitaji pia viungo wa aina ya Gerson Fraga au Tonombe Mukoko ambao wakati mwingine wanaweza kuusoma mchezo na kuwasaidia washambuliaji kufunga. Wanajua njia za mpira.

Jonas na kadi zake

Advertisement

Mashabiki waliondoka uwanjani wakiwa wanamlaumu Jonas Mkude kwa kadi yake ya kijinga. Ndio ilikuwa kadi nyekundu yenye sura mbili. Sura ya kwanza ni Mkude kupunguza jazba za kijinga uwanjani. Aliwahi kupewa kadi nyekundu katika pambano fulani la Simba na Yanga kwa sababu kama ya juzi. Ajipime na kugundua umuhimu wake katika mechi muhimu. Anapoondoka uwanjani timu inapwaya. Inabidi adhibiti hasira. Lakini subiri kwanza, vipi kuhusu Martin Sanya? Nilisema hapo awali kwamba hakuwa na urafiki na wachezaji. Mastaa wengi, hasa wa Stars walikuwa na kinyongo kwa zile tabia ambazo alimuonyesha Samatta hapo awali. Sanya ndiye aliyewapandisha joto kina Mkude uwanjani. Hii ndio sura ya pili.

Hatuna Samatta wala Msuva mwingine

Kocha wa Taifa Stars, Ettiene alijaribu kupanga kikosi bora ambacho kiliondoka bila ya matokeo uwanjani. Shabiki mmoja alisikika akisema: “Sawa mimi ni shabiki wa Yanga lakini kwa nini kocha hakumuingiza Mzamiru Yassin mapema?” Unaishia kucheka tu. Angeanzishwa Mzamiru shabiki huyuhuyu angehoji: “Kwanini Mkude hajapangwa?” Ndivyo mashabiki wetu walivyo. Ukweli ni kwamba kocha alichezesha kikosi bora sana uwanjani. Sioni wachezaji wengi walio nje ya uwanja ambao wangeweza kuiokoa timu kuliko hawa kina Samatta na Msuva. Safu yetu ya ulinzi ilikuwa bora sana kwa maana ya walinzi bora wanaotamba kwa sasa katika ligi yetu. Bakari Mwamunyeto bonge la beki, Abdalah Kheri bonge la beki na pembeni walikuwepo mabeki bora wa pembeni wa ndani kwa sasa, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’. Unadhani kuna wachezaji wengine nje ya hawa? Tuna muda mchache kabla ya kucheza na Tunisia. Tusidanganyane kwamba kuna wachezaji wengine wanaweza kufanya maajabu. Kocha apewe moyo na tuendelee kusimama nyuma ya Stars. Tuache lawama za kulazimisha.

Nyasi za MKAPA tumuachie Mungu tu

Uliziona nyasi za Uwanja wa Mkapa juzi? Lakini hapo hapo tofauti ilikuwa wapi na shughuli nyingine kama ile ya 9 Desemba? Watu wangekaa tu katika majukwaa na wangeiona shughuli vyema. Nadhani haitatokea tena.

 

Advertisement