Taifa Stars kufa au kupona Afrika Kaskazini

Muktasari:

Kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije amesema kikosi chake kipo kamili kwa sasa baada ya kusafiri kwa umbali wa saa 11 kutoka Dar es salaam mpaka Tunisia wakipitia nchini Uturuki kabla ya kurudi tena Afrika na ameahidi kuondoka na ushindi kama kila kitu kitakwenda sawa.

TAIFA Stars leo itatupa karata yake ya pili katika mechi za kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika 2021 katika pambano dhidi ya Libya linalotazamiwa kuchezwa katika dimba la Mustapha Ben Jannet eneo la Monastir nchini Tunisia.

Stars iliwasili nchini Tunisia ambako ni makazi ya muda ya timu ya taifa ya Libya Jumamosi jioni kwa ndege ya Shirika la Ndege la Uturuki na imeweka kambi katika mji wa Sousse uliopo kilomita 253 kutoka mji mkuu wa Tunisia, Tunis.

Kuelekea katika pambano la leo, Stars ambayo imeweka kambi yake katika hoteli ya kifahari ya Movenpick itaongozwa na staa wake anayekipiga katika klabu ya Genk, Mbwana Samatta pamoja na nyota wengine wawili wanaoongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, Simon Msuva anayekipiga Difaa Jadida ya Morocco na Farid Mussa wa Tennerife ya Hispania.

Kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije amesema kikosi chake kipo kamili kwa sasa baada ya kusafiri kwa umbali wa saa 11 kutoka Dar es salaam mpaka Tunisia wakipitia nchini Uturuki kabla ya kurudi tena Afrika na ameahidi kuondoka na ushindi kama kila kitu kitakwenda sawa.

“Nimekuja kutimiza falsafa yangu ya soka ambayo wachezaji wanaielewa. Tumekuja hapa kwa ajili ya kushambulia na kupata ushindi. Nimeongea na wachezaji na wamenielewa. Wanajua tunachotaka. Tukishinda hii mechi tutakuwa tumeingiza mguu mmoja katika kufuzu,” alisema Ndayiragije ambaye ni raia wa Burundi.

Ndayiragije ambaye anawakosa mastaa wake wawili, Erasto Nyoni na Jonas Mkude ambao wamekuwa panga pangua katika kikosi chake, amedai kwamba hana wasiwasi na suala hilo na ni wakati wa wachezaji watakaochukua nafasi zao kuonyesha uhodari wao.

“Ni kweli Nyoni na Mkude wanacheza nafasi za ulinzi na ni wachezaji muhimu, lakini nataka wachezaji watakaocheza nafasi zao waonyeshe kwamba wanastahili kucheza timu ya taifa. Lakini pia falsafa yangu ya ulinzi ni ya sisi kukaa na mpira muda mrefu,” aliongeza kocha huyo.

Naye nahodha Samatta ambaye alipoteza nafasi ya wazi katika pambano dhidi ya Guinea ya Ikweta amedai kwamba hajali sana kama atafunga au vinginevyo lakini anaamini kitu cha muhimu zaidi ni matokeo mazuri kwa Stars.

“Nitajitahidi sana. Nitajaribu kufuta makosa ya pambano la Guinea ya Ikweta lakini kitu cha msingi zaidi ni ushindi kwa Taifa Stars. Hii ni mechi muhimu kwetu kwa sababu ili ufuzu michuano kama hii kuna pointi ambazo inabidi tukusanye ugenini,” alisema Samatta.

Kwa upande wa Libya, kocha wao, Faouzi Benzarti ambaye ni raia wa Tunisia amemuita kipa, Mohamed Al-Forgany katika pambano hili baada ya staa huyo kukosekana katika kikosi cha Libya kwa kipindi cha miaka nane iliyopita.

Libya wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza pambano lao la kwanza dhidi ya Tunisia ambalo lilichezwa jijini Tunis wakipokea kichapo cha mabao 4-1 na hivyo kujikuta wakishika mkia katika kundi la J.

Pambano la leo linatazamiwa kuanza saa mbili usiku kwa saa za Tunisia ikiwa ni saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki na kati na linatazamiwa kuchezeshwa na waamuzi kutoka Malawi ambapo mmoja kati ya waamuzi hao ni mwamuzi wa kike wa CAF, Bernadettar Kwimbira.

Waandishi wa Libya wawavaa Samatta, Msuva

Waandishi wa habari wa Libya juzi walijikuta katika mbio za kuwasaka mastaa wawili wa soka la Tanzania, Mbwana Samatta na Simon Msuva wakati wa mazoezi ya kikosi cha Taifa Stars katika uwanja wa FC Kantouni jijini Sousse nchini Tunisia.

Waandishi hao walionekana kuwa na shauku kubwa ya kuwahoji zaidi Samatta na Msuva wakati walipowasili katika uwanja wa mazoezi kwa ajili ya kupata mahojiano kutoka kwa wachezaji wa Stars lakini wengi walionekana kuwavaa zaidi Samatta na Msuva.

Mwandishi mmoja aliyefahamika kwa jina la Al Ahmed Abdula anayeishi Bengazi nchini Libya alidai kwamba shauku yake kubwa ilikuwa ni kufanya mahojiano na Samatta ambaye wiki chache zilizopita alifunga bao katika pambano la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kati ya timu yake Genk dhidi ya Liverpool.

“Namuona Samatta amevaa jezi namba 10. Nahitaji kufanya naye mahojiano kwa sababu najua ni mchezaji muhimu zaidi katika kikosi chenu na niliona bao lake dhidi ya Liverpool pale Anfield. Mimi ni shabiki wa Liverpool,” alisema Abdula.

Mashabiki hao pia walionekana kuwa na hamu ya kumuona Msuva ambaye wamemsikia kwa muda mrefu akicheza katika Ligi Kuu ya Morocco katika klabu ya Difaa Jadida akiwa ni mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kutamba maeneo ya Afrika Kaskazini.

Timu 2 kutoka katika kila kundi miongoni mwa makundi 12 zitafuzu Afcon.