Taifa Stars, Cape Verde waigombania Dar es Salaam

Saturday October 13 2018

 

By Edo Kumwembe

Praia, Cape Verde: Dakika chache baada ya Taifa Stars kupokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa timu ya Taifa ya Cape Verde timu hizo zimegongana katika uwanja wa Ndege wa Nelson Mandela jijini Praia zikipanda Ndege kuelekea Dar es Salaam
Wakati Stars walitazamiwa kutumia Ndege ya kukodi ya Fastjet, Cape Verde wao walitazamiwa kupanda Ndege ya Air Morocco ambayo ingewafikisha mpaka nchini Morocco kwa ajili ya kuunganisha Ndege ya kuelekea Dar es salaam
Hata hivyo Stars wanatazamiwa kutua Tanzania mapema zaidi kuliko Cape Verde ambao wanaweza kutumia saa 24 hewani huku wakiunganisha ndege katika vituo viwili.
Katika uwanja wa Ndege wa Nelson Mandela hali ilikuwa shwari baina ya misafara ya timu hizo mbili ambapo wachezaji wa Stars na mashabiki walioandamana na timu hiyo walionekana kuwa na huzuni huku wale wa Cape Verde wakionyesha heshima kwa kukaa kimya.
Taifa Stars imekubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Cape Verde katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Capo, Mjini Praia.
Cape Verde inayoshika nafasi 67, katika viwango vya ubora wa soka wa Fifa ikiwa nyumbani ilipata mabao yake mawili ya haraka yaliyofungwa na mshambuliaji Ricardo Gomes kabla ya Yanique Tavares kuhitimisha kwa bao tatu.
Mshambuliaji wao, Ricardo Gomes anayekipiga nchini Serbia katika klabu ya Rartizan ndiye alipachika mabao hayo katika dakika ya 16 na 23 akitumia vizuri uzembe wa mabeki wa Stars, David Mwantika na Hassan Kessy, kabla ya Tavares kumalizia la tatu dakika ya 84 kwa kichwa.
Katika mchezo huo, Ricardo aling'ara kutokana na kiwango bora alichokionyesha alitolewa nje dakika ya 54, baada ya kupata maumivu.
Washambuliaji Stars wakiongozwa na nahodha Mbwana Samatta walishindwa kabisa kutumia nafasi chache walizopata kupata mabao.
Safu ya kiungo ya Stars iliyoingia kucheza kwa kujilinda walikosa umakini na kuwaacha wenyeji Cape Verde kutawala eneo la kati.
 Kipa wa Stars, Aish Manula alifanya kazi ya ziada kuokoa hatari kadhaa langoni mwake kuepusha aibu ya mvua ya mabao.
Kutokana na matokeo hayo, Cape Verde inapanda mpaka nafasi ya kwanza ya Kundi L iliyokuwa inakaliwa na Uganda 'The Cranes' kwa kuwa na idadi kubwa ya mabao, Lesotho ya tatu na Taifa Stars inashika mkia.
Cape Verde na Uganda wana pointi nne. Uganda watacheza mchezo wao wa tatu leo Jumamosi na Lesotho.
Kikosi cha Taifa Stars:
Aishi Manula, Hassan Kessy, Gadiel Michael/ Shomari Kapombe, David Mwantika/ Ally Sonso, Agrey Morris, Abdi Banda, Himid Mao, Mudathir Yahya/ John Bocco, Simon Msuva, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

Advertisement