TUJIKUMBUSHE: Simba mambo yamenoga

SIKU moja baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba ilifanya mkutano wa mabadiliko ya Katiba na Muundo wake uliofanyika Mei17, 2018 katika Ukumbi wa Mwlaimu Nyerere, jijini Dar es Salaam huku Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’ akitajwa kuwa mwekezaji pekee aliyekuwa anawania kuwekeza ndani ya klabu hiyo.

Mo Dewji alitangaza nia ya kuwekeza Sh 20 bilioni ndani ya Simba baada ya kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo kutoka wanachama kwenda mfumo wa hisa (kampuni).

Kwenye mchakato huo ambapo baada ya kukamilika Mo Dewji alipita na kupewa uwekezaji wa asilimia 49 huku asilimia 51 zikiwa za wanachama wa Simba.

Wanachama wa Simba walihitimisha sherehe zao za ubingwa waliokabidhiwa mbele ya Rais Dk John Magufuli pale uwanja wa Taifa ambapo, mabingwa hao watetezi walipewa ubingwa huo huku wakipokea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, bao lililofungwa na Christopher Edward.

Mwanasheria aliyesimamia mchakato huo wa mabadiliko ya Katiba, Evodius Mtawala ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Simba, alisema wanakwenda pamoja na mwekezaji kutengeneza kampuni.

“Tutakuwa na kampuni binafsi (Private Company) ambayo ina sheria zake na wana hisa wanatakiwa angalau wawili na wasizidi 50, lakini wanachama wa Simba wapo zaidi ya 16,000.

“Kwenda na mfumo wa kisheria kwa upande wa wanachama, wanapata muunganiko wa taasisi ambayo kupitia umoja huo watapata nafasi ya kumiliki hisa ambayo itaitwa Simba Sports Club Board Company Limited,” alisema Mtawala

Mchanganuo huo utawafanya wanachama wa Simba kumiliki hisa za timu hiyo kwa asilimi 51 huku mwekezaji akimiliki kwa asilimia 49.