TIMUA VUMBI : Maandalizi mnayofanya tuone matunda uwanjani

Friday July 26 2019

 

By Mwanahiba Richard

KLABU mbalimbali za Ligi Kuu Bara zimeanza maandalizi kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, na pia kuna ambazo zimeingia kambini kabisa na wengine hufanya mazoezi yao wakitokea nyumbani. Yote kwa yote ni maandalizi.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba SC wenyewe wapo Afrika Kusini, ilhali Yanga wamepiga kambi yao mjini Morogoro huku timu zingine pia zikiendelea na maandalizi yao.

Timu nne ambazo ni wawakilishi wa michuano ya kimataifa zenyewe zinapaswa kujiandaa kikamilifu kwani michuano hiyo inaanza sambamba na Ligi Kuu Bara.

Tayari ratiba za michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Simba na Yanga zitashiriki ilitoka pamoja na ratiba ya Kombe la Shirikisho la Afrika ambayo pia inawakilishwa na Azam FC na KMC nayo ilitoka.

Vikosi vyote hivyo vimesajili nyota wapya ambao kwa asilimia zaidi ya 50 ni wapya, hivyo ni kazi kwa makocha kutengeneza muunganiko mzuri wa kuwapa matokeo bora msimu ujao wa michuano hiyo.

Wakati timu zote zinahitaji kufanya vizuri msimu ujao, mashabiki walio wengi wanapenda kuziona timu zao za Simba na Yanga zinaonyesha ushindani mkubwa kwa mambo mawili - usajili na kambi zao.

Advertisement

Simba na Yanga ukiachana na Azam pamoja na KMC ambazo zilishiriki mashindano ya Kombe la Kagame, zenyewe ziliingia kambini mapema na ndio maana zilishindwa kushiriki michuano ya Kombe la Kagame kwa kuhofia ratiba hiyo ya CAF pamoja na Ligi Kuu.

Ukiachana na kambi hizo, pia kila mmoja ana hamu ya kuwaona nyota wao wapya wanafanya nini kwenye michuano hiyo kitu ambacho kila ligi inapoanza hutarajiwa kuonwa na mashabiki pamoja na wanachama.

Simba imesajili nyota mbalimbali kutoka nchi tofauti hivyo hivyo Yanga, Azam FC na KMC ingawa timu hizi mbili usajili wake hautishi sana kutokana na jinsi zinavyojiendesha ukilinganisha na timu hizo kongwe nchini.

Simba iliyo chini ya kocha Patrick Aussems itakuwa na kazi kubwa ya kutengeneza kikosi imara kama ilivyokuwa msimu uliopita ambapo waliweza kufuzu hadi hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa pamoja na kutetea ubingwa wa Ligi Kuu.

Nyota wengi wa kigeni wameingiza kwenye kikosi cha Simba ukiachana na wale watatu pekee waliokuwepo msimu uliopita ambao ni Meddie Kagere, Paschal Wawa, Clatus Chama huku wengine wapya wa kigeni wakiwa sita.

Muunganiko wa msimu uliopita ni lazima utakuwa tofauti na msimu ujao kwa nyota hao inaweza kuwa bora zaidi ama mbovu hayo yote yanategemewa na jinsi walivyojiandaa huko Sauzi vivyo hivyo kwa Yanga ambayo msimu uliopita ilipambana kutwaa ubingwa lakini safari yao iliishia njiani.

Safari ya Yanga haikuwa ndefu sana kutokana na maizngira ya klabu yalivyokuwa msimu uliopita, hali mbaya ya kiuchumi pamoja na kikosi chao ambapo wachezaji wengine walikuwa ni walewale waliocheza mechi zote, ambapo mmoja akiumia lazima pengo lionekane tofauti na ilivyokuwa kwa watani zao Simba, ambao walicheza kwa kujinafasi hata kama wakiwa na mechi nyingi.

Hivyo basi msisimko wa mafanikio ya timu hizo kwa msimu ujao unategemewa kuwa mkubwa baada ya Yanga kusajili wachezaji wenye uwezo na hata uongozi kupambana kutafuta pesa kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo wanachama wao.

Mengi mazuri yanatarajiwa kwa timu hizo nne na nyingine zote zinazojiandaa na ligi hiyo kwani nazo huenda zinajipanga jinsi ya kufanya vizuri na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Inatarajiwa kwamba timu hizo zitarudi na mambo mapya na yenye ushindani kwenye soka, mambo ya kiufundi na kufuata kanuni zote za soka, hakutakuwa na visingizio kwa timu hizo kwamba zilichelewa kuanza maandalizi kwani viongozi wao wamejitahidi kwenda na ratiba.

Makocha wao walipendekeza maandalizi yaanze lini na wapi, jambo hilo limefanywa kwa kiwango kikubwa na viongozi wa timu hizo, sasa hapo kazi imebaki kwenye utekelezaji kupitia makocha na wachezaji.

Matumaini ya wengi kama nilivyoeleza msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kuwa na ushindi mkubwa kutokana na usajili wa timu shiriki lakini pamoja na kufanya vizuri michuano ya kimataifa inayoshiriki timu hizo. Hivyo maandalizi yao yataonyesha matunda uwanjani.

Akili za wachezaji nazo zinahitaji kutulia, kufuata maelekezo ikiwemo kujiongeza uwanjani hasa pale watakapokuwa wanaona mambo yamewaelemea na sio kusubiri mwongozo pekee wa makocha wao ambao kazi yao inakuwa imeishia mazoezini.

Kwa kuangalizia vikosi hivyo kuna wachezaji wazoezi na wale ambao wanachipukia ambapo itahitajika pia uvumilivu wa kuzoea mfumo mzima wa timu ingawa hiyo sio sababu ya kushindwa kuonyesha kile walichokipata kutoka kwenye kambi zao hizo za muda mrefu.

Kila jambo linawezekana, lakini katika uga wa michezo tunaambiwa na ndivyo ilivyo, maandalizi mazuri huzalisha mafanikio makubwa uwanjani, jambo ambalo hata kwa timu zetu zinapaswa kuhakikisha kwamba zinafanya hivyo ili kufikia malengo.

Ni wazi na bayana kwamba, maandalizi mazuri hayamuachi mtu bila mafanikio.

Advertisement