THE ROCK: Mwili nyumba mwenye mkwanja mrefu

FLORIDA MAREKANI. MWITE The Rock, maana ndivyo wanavyomwita hivyo kwa jina lake la ulingoni. Dwayne Douglas Johnson ndio jina alilopewa na wazazi wake. Ushamjua?

Ni yule mwigizaji wa Marekani, mtayarishaji na staa wa kulipwa wa zamani wa mchezo wa mieleka. Johnson alikuwa mcheza mieleka wa WWF, ambako ndiko alikopata jina la The Rock. Lakini, kwa miaka minane, The Rock ameamua kujikita kwenye kuigiza. Filamu zimezidi kumpa umaarufu na mkwanja mrefu zaidi.

The Rock, aliyezaliwa Mei 2, 1972 akiwa na umri wa miaka 47, anatajwa kuwa mmoja kati ya watu wenye pesa ya kutosha huko Hollywood. Kwa mujibu wa Forbes, The Rock aliingiza pesa nyingi sana mwaka jana, kiasi kinachomfanya kuboresha kipato chake na kuwa cha kibosi zaidi. Staa huyo wa filamu anatajwa kuwa na pato la Dola 220 milioni. Ndio, Dola 220 milioni.

Mkwanja wa The Rock

Kwenye orodha ya wacheza filamu 10 waliolipwa pesa nyingi zaidi kwa mwaka uliopita, kwa mujibu wa Forbes, The Rock aliweka kibindoni Dola 89.4 milioni na kuwa namba kwa waingizaji waliopiga mkwanja mrefu Forbes inadai kwamba The Rock alipokea Dola 23.5 milioni kwenye filamu ya Jumanji: Welcome to the Jungle. Kwa ujumla wake, The Rock kwa mwaka 2018, aliweka mfukoni Dola 124 milioni.

Kwa mujibu wa The Richest.com, The Rock ameripotiwa kuwa na pato linalofikia Dola 280 milioni. Forbes wao wanamtaja mkali huyo wa filamu mwenye mwili jumba kuwa na pato la Dola 165 milioni.

Ukiweka kando filamu, sehemu nyingine ambayo The Rock amekuwa akipiga pesa kupitia dili za matangazo ya kibiashara ikiwano Under Armour. Hivi karibuni, The Rock alitangaza kununua hisa Voss Water, hivyo jambo hilo linamfanya kuwa mmiliki.

Nyumba na usafiri

Ukiwa na pesa unaishi unavyotaka na unamiliki unachokitaka, kwa kuwa tu kinapatikana kwa kununuliwa. Makazi ya The Rock ni matata. Jumba lake la huko Florida linaripotiwa kuwa na thamani ya Dola 3.4 milioni. Jumba hilo lina vyumba vya kulala, mabafu, ukumbi wa sinema, gym, bwawa la kuogelea na bustani iliyotengenezwa kwa pesa nyingi sana. The Rock, ambaye alitamba pia kwenye filamu za Fast & Furious 6, alinunua jumba hilo kutoka kwa Vernon Carey. Huwezi kuwa na pesa ndefu, kuishi kwenye jumba la kifahari, kisha ukamiliki usafiri wa hovyo hovyo. Ukienda kwenye maegesho ya The Rock, ndinga unazokutana nazo huko si mchezo. Baadhi ya magari tu ya kifahari ya staa huyo ni pamoja na Ford F-150, ambayo bei yake inaanzia Dola 50,000. Hennessey VelociRaptor V8 inayouzwa Dola 150,000, Pagani Huayra Dola 1 milioni, Ferrari LaFerrari Dola 1.15 milioni, Rolls Royce Wraith Dola 258,000.

Uhusiano na familia

Staa Dwayne ‘The Rock’ Johnson hivi karibuni alifunga ndoa na mpenzi wake wa siku nyingi, mrembo Lauren Hashian. Mke huyo wa sasa wa The Rock ni mwimbaji, mtunzi, mtayarishaji wa muziki, ambaye amekuwa moto tangu alipokuwa na umri wa miaka 19. Mrembo Lauren anatokea kwenye familia ya wanamuziki, baba yake alikuwa mpiga dramu wa Bendi ya Boston na mama yake pia amekuwa maarufu kupitia tasnia hiyo ya muziki. Hata hivyo, Lauren ni mke wa pili wa The Rock kwenye maisha yake, kwani huko nyuma alikuwa na mrembo Dany Garcia na kuachana naye. Mrembo Dany anaripotiwa kuwa na mchango mkubwa katika maisha haya ya sasa ya mkali huyo wa filamu, The Rock.