TFF yazitupa Yanga, Simba usiku

Muktasari:

Huu ni msimu wa tano wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam kuchezwa huku Yanga, Simba na Azam kila moja ikitwaa ubingwa mara moja

Mechi mbili za hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika zitakazohusisha timu za Yanga, Simba na Azam FC zitachezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini kesho kuanzia saa 1.00 usiku.

Kwa mujibu wa ratiba ya hatua hiyo iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), mechi zote zitakazochezwa Uwanja wa Taifa zitafanyika usiku na zile za viwanja vingine zitachezwa kuanzia saa 10.00 jioni.

Mchezo wa kwanza utakaochezwa usiku ni ule wa Yanga dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa kesho kuanzia saa moja kamili usiku.

Mechi hiyo itatanguliwa na ile ya Namungo FC dhidi ya Alliance ambayo imepangwa kuchezwa kuanzia saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Kassim Majaliwa huko Ruangwa Lindi.

Jumatano kutakuwa na mchezo mwingine baina ya Simba na Azam FC ambao nao utachezwa katika uwanja wa Taifa.

Kabla ya mechi hiyo, mkoani Tanga kutakuwa na pambano baina ya wenyeji Sahare All Stars dhidi ya Ndanda FC utakaochezwa kwenye uwanja wa Mkwakwani.

Ifahamike kwamba Sahare All Stars ndio timu pekee ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) iliyobakia katika mashindano hayo.