TFF yawatega Mkude, Morrison

Muktasari:

Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa kanuni ya 37 ya udhibiti wa wachezaji kipengele cha tano (5) kwa kosa linalofanana na lile la wachezaji hao kupiga viwiko wachezaji wa timu pinzani.

Dar es Salaam. Huruma ya Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ndio pekee inayoweza kuwafanya wachezaji Jonas Mkude na Bernard Morrison kucheza mechi ya watani wa jadi, Yanga na Simba, Machi 8 mwaka huu jijini.

Wachezaji hao wawili wapo katika uwezekano mkubwa wa kukosa mchezo huo kutokana na adhabu ya kufungiwa mechi tatu na faini ya Shilingi 500,000 kwa kila mmoja kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu waliyofanya katika mechi mbili tofauti za timu zao.

Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa kanuni ya 37 ya udhibiti wa wachezaji kipengele cha tano (5) kwa kosa linalofanana na lile la wachezaji hao kupiga viwiko wachezaji wa timu pinzani.

“Mchezaji atakayefanya jambo lolote kati ya yafuatayo atafungiwa michezo isiyopungua mitatu (3) na faini isiyopungua Sh. 500,000 (laki tano).

Kupigana/kupiga kabla, wakati wa mchezo au mara tu baada ya mchezo kumalizika,” kinafafanua kifungu cha 5(2) cha kanuni hiyo.

Mghana Bernard Morrison wa Yanga anayecheza nafasi ya winga, amepelekwa mbele ya kamati hiyo kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Tanzania Prisons FC, Jeremia Juma katika mchezo uliofanyika Februari 15, 2020 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baina ya timu hizo.

Naye kiungo wa Simba, Jonas Mkude amepelekwa katika kamati ya nidhamu kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Biashara United FC, Ally Kombo katika mchezo uliofanyika Februari 22, 2020 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Wakati ikiwa haijulikani hasa kamati hiyo chini ya Wakili Kiomoni Kibamba itakutana lini kuwajadili, uwezekano wa wachezaji hao kucheza au kutocheza mechi hiyo utategemea na siku ambayo kamati hiyo itakaa.

Afisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo alisema kamati hizo zipo huru na zinafanya kazi muda wowote endapo namba ya wajumbe itakuwa imekamilika licha ya changamoto zinazoikumba.