TFF yapewa kiwanja Kigamboni

Muktasari:

 Juni 15, Makonda aliahidi kuipatia Yanga, kiwanja eneo la Kigamboni na kwa sasa tayari taratibu za kuwamilikisha kisheria zimeshaanza. 

Dar es Salaam. Ikiwa ni siku tano tu zimepita tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutangaza kuikabidhi Yanga, uwanja huko Kigamboni, neema kama hiyo imeangukia kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Makonda leo ameahidi kulipatia shirikisho hilo kiwanja chenye ukubwa wa ekari 15 huko Kigamboni ili liweze kujenga kituo cha soka.

Akizungumza kwenye hafla ya kuichangia timu ya taifa 'Taifa Stars' iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo, Makonda alisema TFF itapatiwa zawadi hiyo kama sehemu ya mchango wa kamati ya Hamasa ya Taifa Stars.

"Mheshimiwa Makamu wa Rais tupo hapa kuichangia Taifa Stars, lakini ieleweke kwamba kampuni na taasisi zilizochangisha fedha zote ziko ndani ya mkoa wangu na zimewawakilisha wananchi wa Dar es Salaam.

“Pamoja na hilo natambua kazi kubwa inayofanyika hivyo binafsi mchango wangu ni kuipatia TFF kiwanja cha ekari 15 ili iweze kujenga kituo cha soka na bahati nzuri Rais wa shirikisho ameniambia hapa kuwa fedha zipo kutoka FIFA ambazo zitatumika katika ujenzi wa kituo hicho," alisema Makonda