TFF: Tunafuatilia tukio la rushwa upangaji matokeo

Muktasari:

Jana Ijumaa zilikuwa zikisambaa picha mtandaoni zikionyesha tukio la viongozi wa timu hizo katika mazingira ya kutoa rushwa ya upangaji matokeo.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema kwamba limepata taarifa ya tukio la rushwa ya upangaji matokeo katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza  kati ya Rhino Rangers ya Tabora na Dodoma FC.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi, imeeleza kwamba TFF inaendelea kufuatalia kwa karibu, na itawasiliana na mamlaka zinazofanya kazi ya uchunguzi nchini kubaini ukweli wa jambo hilo.

“Tutakapobaini kulikuwa na nia ya kupanga matokea hatua kali zitachukuliwa kwa wahusika kwa mujibu wa kanuni na taratibu,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Ofisa Habari wa Shirikisho hilo, Cliford Ndimbo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa wakati huu ambao TFF inafuatilia inawaomba wapenzi wa mpira wa miguu kuliacha suala hili kwa mamlaka husika.

Awali, jana Ijumaa zilikuwa zikisambaa picha mtandaoni zikionyesha tukio la viongozi wa timu hizo katika mazingira ya kutoa rushwa ya upangaji matokeo.