Sven aunguruma Samora, Lipuli wajipanga

Muktasari:

Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, ameweka wazi kuwa kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wao wa leo Jumamosi dhidi ya Lipuli FC.

KOCHA wa Simba, Sven Vandenbroeck, ameweka wazi nyota wake 25, wako tayari kuwavaa Lipuli FC ya Iringa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.
Simba ambao ni vinara wa Ligi Kuu Bara wakiongoza na pointi 53, wakiwa wamecheza mechi 21, Azam FC wa pili wana 44, wamecheza mechi 21 na Yanga wakiwa wa tatu na pointi 38 wakicheza mechi 19.
Watakuwa ugenini mbele ya 'Wanyarukolo' hao kuwania pointi tatu muhimu ambazo zitamsaidia kufikisha malengo yake ya kutetea ubingwa.
"Kila mchezaji yupo tayari kwa mchezo wa leo. Tulisafiri na wachezaji 25 na wote wapo tayari. Lazima tucheze kila mchezo kwa nguvu katika kila hali ambayo tunakutana nayo kuhakikisha tunafanya vizuri," alisema Sven.
Kocha wa Lipuli FC, Julio Helieza, alisema wanaiheshimu Simba ni timu kubwa na zoefu lakini wamejiandaa kuona wanashinda.
"Tutakuwa kwenye uwanja wa nyumbani lengo ni kupambana kwa nguvu zote kuona tunaibuka na ushindi,"alisema Julio.
MIRAJI, MDHAMIRU HALI TETE
Mbelgiji huyo aliyewahi kuzifundisha timu tofauti ikiwemo ya timu ya Taifa ya Zambia 'Chipolopolo' ameweka wazi kuwa wachezaji wake wawili, Miraji Athuman na Mzamiru Yassin hali zao bado.
"Tutaendelea kuwakosa majeruhi wa muda mrefu Mzamiru na Miraji ambao walibaki Dar es Salaam wakiendelea kujiuguza,".