Sven ataka mabadiliko kabla ya Ligi ya Mabingwa Afrika

Muktasari:

Simba inaondoka leo Septemba 10 kuifuata Mtibwa Sugar mkoani Morogoro.

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Sven Vandebroeck amewaambia wachezaji wake kuwa wanapaswa kuongeza kasi na kukusanya pointi zaidi kabla ya kuanza mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba imekuwa ikipata tabu katika mechi za kimashindano msimu huu kuliko ikiwa katika michezo ya kujipima nguvu.
Imefanya vizuri katika michezo kadhaa kama ule dhidi ya KMC wakishinda mabao 3-1-, na kisha kuichapa Transit Camp 5-2, michezo yote hiyo ikiwa ya kujipima nguvu.
Simba iliifunga Vital’O ya Burundi mabao 6-0 katika mchezo wa Siku ya Simba, lakini ikaifunga Namungo 2-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii.
Mabingwa hao waliichabanga AFC mabao 6-0 katika mchezo mwingine wa kirafiki, lakini hali ilibadilika dhidi ya timu ndogo ya Ihefu katika Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kupata ushindi wa mabao 2-1.
Akizungumza jana, Sven alisema wanatakiwa kuendelea walipoishia msimu uliopita ii kuhakikisha wanashinda mechi nyingi na kutwaa tena ubingwa msimu huu.
Simba ilianza vizuri Ligi Kuu Bara kwa ushindi wa mabaoi 2-1 ingawa mashabiki wa timu hiyo waliwalaumu wachezaji wakidai walicheza chini ya kiwango.
Simba inatarajia kuondoka leo kwenda mkoani Morogoro kwa ajili ya mchezo wao wa pili wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar, utakaofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Kocha huyo raia wa Ubelgiji anatambua kuwa Ligi ya Mabingwa Afrika ikianza, mambo yanakuwa mengi, ndiyo maana anataka pointi nyingi katika mechi zote watakazocheza kuanzia Jumamosi.
“Baada ya kuwa na msimu mzuri uliopita, ningependa kuwaona wachezaji wangu wakiwa bado na uchu. Ukishinda mataji mengi uchu wa mafanikio unaondoka, hivyo akili kuelekezwa kwenye mechi kubwa na kusahau ligi.
“Kwetu tunataka kuendelea tulipoishia na kuwa na ari ileile kwenye kila mechi. Unaweza kuchukulia rahisi katika mechi za mwanzo kwa kuona bado mnapasha lakini kiuhalisia ni hapana,” alisema Sven.
Aliongeza: “Tunapaswa kukusanya pointi nyingi kadri tuwezavyo kabla ya ligi ya Mabingwa Afrika kuanza, tunatakiwa kuwa na uhakika pia wa kuua mechi mapema.
“Ukweli wachezaji na mashabiki tulikuwa na msimu mzuri uliopita, tulishinda mataji yote ya ndani na bila shaka kila mtu alikuwa na furaha, lakini mashabiki waelewe ni ngumu kupata makombe yote kila msimu,” alisema Sven.
Kocha wa zamani wa Prisons, Mohammed Adolph Rishard aliunga mkono kauli ya Sven kwa kusema kuwa tabia ya kiasili ya binadamu ni kubweteka pindi tu anapopata mafanikio.
“Yuko sahihi kabisa na wachezaji wanatakiwa kutambua hilo kwamba licha ya kupata mafanikio hawatakiwi kubweteka, wapambane na isitoshe ndiyo timu itakayoiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa.
“Sasa kama wachezaji wanatakiwa wasilaze damu, lakini pia kocha anajihami mapema kuwa mafanikio makubwa waliyoyapa msimu uliopita yasiwe kama kitanzi kwao, kwamba ikitokea mfano wakapata matokeo mabaya katika baadhi ya mechi basi wajue kuwa ni kawaida kwani timu nyingi zitawakamia msimu huu,” alisema Rishard.
Kocha Mrage Kabange alisema Simba wanatakiwa kujipanga hasa msimu huu kama wanataka kweli kuchukua tena ubingwa kwani timu nyingi zitakuwa zinawakamia.
“Kocha Sven ameongea kitu cha ukweli, kwani timu nyingi zikishapata mafanikio zinapata wakati mgumu kurudia mafanikio hayo msimu mwingine kwa sababu kwanza zinakamiwa na wapinzani wao, lakini pia wakati mwingine zinabweteka.
“Angalia mfano Liverpool, imetwaa ubingwa wa Englandmsimu uliopita lakini msimu huu sijui kama itabeba tena kombe, maana kila timu inaikamia, lakini pia mashabiki wanatakiwa kujiandaa kisaikolojia na kuondokana na ile dhana kwamba timu kubwa hazistahili kufungwa na timu ndogo, hii ni kushindwa kujua zote zinashiriki ligi moja,” alisema Mrage.