Sure Boy: Azam tunautaka ubingwa

Muktasari:

Kagera Sugar ndiyo iliyoharibu rekodi ya Azam ya kutoruhusu bao katika mechi nne mfululizo tangu msimu huu wa ligi uanze.

BAADA ya ushindi wa tano mfululizo kwa Azam Fc, kiungo wa timu hiyo Salum Abubakary 'Sure Boy' amesema msimu huu wanataka kuwa mabingwa wa Ligi Kuu na sio kitu kingine na ndio maana wanapambana sana kuhakikisha kila mchezo wanapata ushindi.

 "Namshukuru Mungu kwa kupata hizi pointi tatu na kuongoza Ligi, msimu huu tuna jambo letu  kwani tunahitaji sana ubingwa kiukweli" alisema.

 Akizungumzia timu yao kuruhusu goli mbili katika mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar Juzi Jumapili, Sure Boy amesema " Unajua mechi inakuwa ngumu, tumeshinda mechi nne mfululizo na watu wamekuja wanakamia sana hivyo inabidi tuipange sana ka ssa ili tuendeleze kasi yetu ya ushindi".

 Sure Boy alisema katika mechi zilizopita walikuwa wanatengeneza nafasi nyingi lakini kutumika ilikuwa tatizo lakini mwalimu wao alifanyia kazi na ndio maana kwenye mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar idadi ya magoli ya kufunga iliongezeka.

 Akizungumzia mchezo wao dhidi ya Mwadui Fc utakaopigwa Oktoba 15, alisema "Kikubwa sisi kila mchezo kwa yule ambaye tunakutana nae sisi tunataka pointi tatu ".

 Katika kikosi hiko kinachonolewa na kocha Aristica Cioaba, mpaka sasa ndio kimetoa kinara anayeongoza kwa mabao kwenye Ligi Kuu Bara, Prince Dube aliyefunga mabao matano akifuatiwa na Meddie Kagere wa Simba aliyefunga manne.