Suarez mwili Barca, moyo upo Arsenal

Muktasari:

  • Suarez amejiona tayari kama ameshatua Arsenal baada ya kushindwa kuficha mapenzi yake wakati alipoonekana kama vile ameungana na Washika Bunduki hao kushangilia ushindi waliopata mbele ya Chelsea kwenye Ligi Kuu England juzi Jumamosi.

LONDON, ENGLAND.ISHU ya Denis Suarez basi tu Arsenal imeamua kujichelewesha yenyewe. Unaambiwa hivi, staa huyo wa Kihispaniola kwa sasa mwili tu ndio upo Barcelona, lakini akili na moyo wake upo kwenye mpango wa kuhamia Arsenal akakipige kwenye Ligi Kuu England sambamba na washambuliaji matata, Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette.

Ripoti zinadai Arsenal inataka kulipa Pauni 1.7 milioni ili kumchukua Suarez kwa mkopo kwanza kwa makubaliano ya kulipa Pauni 17.5 milioni mwishoni mwa msimu ili kumbeba jumla mchezaji huyo.

Dili hilo bado halijakamilika na kinachoonekana ni Arsenal yenyewe tu ndio inayojichelewesha, lakini mchezaji mwenyewe yupo tayari kwenda kuungana na wenzake kufanya kweli kwenye mchakamchaka wa kuhakikisha timu hiyo inamaliza msimu ikiwa ndani ya Top Four.

Suarez amejiona tayari kama ameshatua Arsenal baada ya kushindwa kuficha mapenzi yake wakati alipoonekana kama vile ameungana na Washika Bunduki hao kushangilia ushindi waliopata mbele ya Chelsea kwenye Ligi Kuu England juzi Jumamosi.

Kikosi hicho cha Kocha Unai Emery kiliichapa Chelsea 2-0 shukrani kwa mabao ya Lacazette na beki wa kati, Laurent Koscielny.

Ligi Kuu England ilituma picha za wafungaji hao wa mabao ya Arsenal kwenye ukurasa wake wa Instagram na Suarez hakutaka kujivunga na kubonyeza kitufe kilichoandikwa ‘like’ ikiwa na maana amesapoti ushindi iliyopata timu hiyo ambayo inahusishwa na mpango wa kumsajili.