Stars watua Ulaya, wageuza Afrika

Saturday November 16 2019

 

By Edo kumwembe

SAA chache baada ya kuichapa Guinea ya Ikweta katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kikosi cha timu ya taifa,Taifa Stars kimewasili jijini Istanbul, Uturuki kwa ajili ya kuunganisha ndege ya kuelekea Tunisia.
Stars wanatazamiwa kucheza na Libya ambayo inatumia Uwanja wa Taifa wa Tunisia kama uwanja wao wa nyumbani kutokana na hali ya amani kuwa shakani nchini mwao.
Stars waliosafiri na ndege ya Shirika la Ndege la Uturuki walitua Istanbul saa tano na dakika 20 na walitazamiwa kuunganisha ndege ya kwenda Tunisia saa saba na dakika 25.
Kocha wa Stars, Etienne Ndayiragije amesema wana uhakika mkubwa wa kupata pointi tatu au moja kutoka kwa Libya baada ya kuzoa pointi zote tatu kutoka kwa Guinea ya Ikweta.
Stars iliinyuka Guinea ya Ikweta mabao 2-1 na Jumanne ijayo inakutana na Libya iliyochezea kipigo cha mabao 4-1 kutoka Tunisia kwenye mechi za Kundi J kuwania Fainali za Afcon 2021.
"Mungu akitujalia tutapata pointi Libya. Kama sio tatu basi hata moja na tutakuwa tumekaa katika nafasi nzuri katika kundi" alisema kocha huyo raia wa Burundi.

Advertisement