Stars vs Burundi, Ni shoo ya Samagoal na Berahimo

KESHO jioni kuna shoo moja matata wakati timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stara’ itakapoikaribisha Ntamba Murugamba ambayo ni timu ya taifa ya Burundi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam katika mechi ya kirafiki kimataifa.

Pambano hilo linalotambuliwa kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka duniani (Fifa), litapigwa saa 10 jioni likiwa la kwanza kwa timu hizo za taifa kuumana tangu kuibuka kwa corona, ambapo timu zote mbili zimewaita mastaa wa maana kwenye mchezo huo.

Maproo wote wa Stars wanaocheza nje ya nchi soka la kulipwa wametua nchini isipokuwa Himid Mao wakiungana na wachezaji wanaocheza ligi za ndani kwa ajili ya mchezo huo.

Wakati majirani, Kenya watakuwa wakiwakaribisha Zambia jijini Nairobi kwenye wiki hii ya kimataifa, Stars itavaana na Burundi ambayo tangu 1971 zmekutana mara 20 na Tanzania kushinda mara 13, kutoka sare mara tatu na kupoteza mara tano.

Kama ilivyo kwa Tanzania ambayo imewaita nyota wake wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, Burundi nayo ikiwa chini ya kocha Olivier Niyungeko Mutombola imeita mashine zake kwa ajili ya mchezo huo.

Tofauti na Tanzania inayonolewa na Etienne Ndayiragije anayetokea pia Burundi iliyowaita wachezaji sita tu wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, zaidi ya nusu ya kikosi cha Burundi kinaundwa na nyota wanaocheza nje ya nchi yao wakiongozwa na nyota wa zamani wa West Bromwich, Saido Berahino anayekipiga katika klabu ya RSC Charleroi ya Ubelgiji.

Huku Samatta na wenzake ambao wamekuwa wakicheza soka la kulipwa nje ya nchi kule atakuwepo Berahino.Hawa hapa maproo wa Tanzania na Burundi ambao wanatarajiwa kuonyesha makali yao kwenye mchezo huo wa kirafiki.

MBWANA SAMATTA

Samatta anayecheza soka la kulipwa Uturuki kwenye klabu ya Fenerbahce, ndiye mshambuliaji hatari zaidi kwenye kikosi cha Taifa Stars.

Anaweza kuwa mchezaji ambaye atakuwa akitazamwa zaidi na mabeki wa Burundi kutokana na mambo makubwa ambayo amekuwa akiyafanya barani Ulaya.

Licha ya kutofanya vizuri akiwa na Aston Villa ya Ligi Kuu England, Samatta anaonekana kurejea kwenye makali yake.

Mshambuliaji huyo alithibitisha hilo Oktoba 3, 2020 kwenye mchezo wake wa kwanza kuanza kwenye kikosi cha Fenerbahce dhidi ya Fatih Karagumruk ambapo alitupia mabao mawili yaliyoipa timu yake pointi tatu za mchezo huo.

SADIO BERAHINO

Ukubwa wa jina la Samatta kwa Tanzania ni sawa na ule wa Berahino huko Burundi, na wawili hao wameonja utamu wa Ligi Kuu ya England. Nyota huyo kwa sasa anacheza soka la kulipwa Ubelgiji. Nahodha huyo wa timu ya taifa la Burundi, alicheza ligi hiyo ya Malkia akiwa na West Bromwich Albion kabla ya kwenda Stoke City ya daraja la Kwanza ‘Championship’.

Tangu kuanza kwa msimu huu Berahino amefunga mabao mawili na kutoa assisti moja kwenye michezo minane aliyoichezea RSC Charleroi kwa mkopo akitokea Zulte Waregem zote za nchini Ubelgiji.

SAIMON MSUVA

Ukimuondoa Samatta, Msuva ambaye anacheza soka la kulipwa Morocco kwenye klabu ya Difaa El Jadida ni mchezaj mwingine wa Kitanzania ambaye amekuwa akiipeperusha vyema bendera ya nchi nje ya nchi. Huu ni msimu wake wa tatu anacheza soka la kulipwa nchini humo na amekuwa akihusishwa na klabu kadhaa barani Ulaya, ikiwemo Le Havre ya Ligi Daraja la Kwanza nchini humo maarufu kama Ligue 2.

Msuva amefunga mabao matano msimu huu kwenye ligi ya Morocco na amekuwa akifanya vizuri akicheza kama mshambuliaji wa mwisho akicheza na Samatta au kutokea pembeni.

BONFILS CALEB

Achana na Sadio Berahino ambaye amekuwa akitumika kama winga na muda mwingine hucheza namba 10, Bonfils Caleb ndio mtambo wa mabao wa Burundi.

Jamaa huyu ndiye anamsugulisha benchi Blaise Bigirimana wa Namungo FC katika timu yao ya taifa. Caleb anacheza soka la kulipwa Slovakia katika Klabu ya Pohronie, na msimu huu wa Ligi Kuu nchini humo maarufu kama Fortuna Liga ameuanza vizuri kwa kutupia mabao matatu kwenye michezo saba.

THOMAS ULIMWENGU

Unaweza kusema kuwa Ulimwengu ndiye mchezaji ambaye ameanza kuonja utamu wa kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kuliko mchezaji mwingine yeyote kwenye kikosi cha sasa cha Taifa Stars.

Tofauti na Msuva pamoja na Samatta, Ulimwengu hakuwahi kucheza Ligi Kuu Bara, amekuwa mtu wa kupasua anga japo mambo yameonekana kutomnyookea kama ilivyo kwa wenzake. Kwa sasa yupo TP Mazembe na ameuanza msimu mpya wa Ligi Kuu nchini humo ambapo wamecheza mchezo mmoja ambao walitoka suluhu dhidi ya Blessing.

MOHAMED AMISSI

Akiwa mzaliwa wa Brussels, Ubelgiji, huyu ni winga ambaye amekuwa akichipukia kwa kasi nchini Uholanzi ambako anacheza soka la kulipwa akiwa na Heracles Almelo ambayo inashiriki Ligi Kuu.

Amissi ambaye anatumia mguu wa kushoto amepata nafasi ya kucheza mchezo mmoja tu kati ya minne ambayo chama lake limecheza kabla ya wiki ya michezo ya kimataifa.

HIMID MAO

Panga pangua kwenye kikosi cha Enppi huko Misri lazima utamuona Himid Mao ‘Ninja’ akianza kikosi cha kwanza cha timu hiyo huku akitumika kama kiungo mkabaji.

Kukosekana kwake kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kunaweza kusababishwa na mambo mawili ambayo ni majeraha au kocha aamue ampumzishe. Himid ambaye alianza kucheza soka la kulipwa nchini Misri akiwa na Petrojet kabla ya kushuka daraja, ni miongoni mwa wachezaji ambao wamekuwa wakitegemewa na Kocha Helmi Toulan kwenye kikosi chake.

PHILIP NZEYIMANA

Tanzania si yupo Shomary Kapombe ambaye amekuwa akifanya vizuri kama beki wa kulia? Sasa Burundi wanaye mchezaji anayeitwa Philip Nzeyimana na amekuwa akifanya vizuri akiwa na Akademisk BK ambayo inashiriki Ligi Daraja la Pili nchini Denmark.

Nzeyimana msimu huu amecheza michezo minne kati ya sita ambayo chama lake limecheza na wapo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.

ALLY MSENGI

Kocha wa Stellenbosch FC, Steve Barker amekuwa akimmwagia sifa kiungo wake Ally Msengi juu ya kipaji kikubwa alichonacho cha kucheza soka na ndio maana amekuwa akimpa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza licha ya umri mdogo alionao.

Msengi mwenye umri wa miaka 18, msimu uliopita alicheza michezo saba na kutajwa kuwa miongoni mwa makinda wanaochipukia kwa kasi kwenye ligi hiyo ambayo kwa sasa inafahamika kama DStv Premiership.

YOUSSOUF NDAYISHIMIYE

Huyu ni habari nyingine akicheza ligi moja na Samatta nchini Uturuki wakati Samagoal akiwa na Fenerbahce, Ndayishimiye anatesa na Yeni Malatyaspor. Kiungo huyo msimu huu amecheza michezo yote minne ya Ligi Kuu Uturuki na kutoa asisti moja kwenye mchezo dhidi ya Göztepe, na amekuwa akitumia muda mwingine kama beki wa kati. Huu ni msimu wa kwanza kwa Ndayishimiye mwenye miaka 21 kucheza soka la kulipwa Uturuki akitokea Aigle Noir FC ya Burundi iliyocheza mchezo wa kirafiki na Yanga kwenye Wiki ya Mwananchi.

NICKSON KIBABAGE

Ni mchezaji kinda mwingine kwenye kikosi cha Taifa Stars ambaye anacheza soka la kulipwa nje ya nchi. Ukiachana na Msengi, Kibabage amekuwa akibadilika kadri siku zinavyosonga na ni tofauti kabisa na yule ambaye alikuwa akikikichezea kikosi B cha Mtibwa Sugar.

Licha ya kutocheza mchezo hata mmoja wa ushindani akiwa na Difaa El Jadida ya Morocco, amekuwa kwenye kiwango cha juu kwa sasa - sio beki tu wa kushoto, amebadilishwa na kuwa winga, anaweza kushambulia na kuzuia.

FREDERIC NSABIYUMVA

Wakati Tanzania kukiwa hakuna beki hata mmoja aliyeitwa kutoka nje ya nchi, Burundi wanaye Frédéric Nsabiyumva ambaye ni beki wa kati anayeipeperusha vyema bendera ya taifa lake Afrika Kusini akiwa na Chippa United.

Nsabiyumva anacheza ligi moja na Watanzania - Msengi na Abdi Banda ambaye hakuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars. Beki huyo wa kati wa Chippa United amecheza michezo 21 msimu ulioisha hivi karibuni huko Afrika Kusini, ikiwemo 18 ya DStv Premiership.

Hao ni baadhi tu ya nyota wa nchi hizi mbili wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi ambao ni tishio, lakini hivi ni vikosi vya timu mbili vilivyoitwa kwa ajili ya mchezo huo wa kirafiki.

TANZANIA

Metacha Mnata (Yanga), Aishi Manula (Simba), David Kissu (Azam), Shomary Kapombe (Simba), Bryson David (KMC), Bakari Mwamnyeto (Yanga),Abdallah Sebo (Azam) na Dickson Job (Mtibwa Sugar). Wengine ni Iddy Mobbi (Polisi Tanzania), Jonas Mkude (Simba), Himid Mao (ENPPI, Misri), Simon Msuva (Difaa El Jadida, Morocco), Ditram Nchimbi (Yanga), Feisal Salum (Yanga). Ally Msengi (Stellenbosch, Afrika Kusini), Mbwana Samatta (Fenerbahce, Uturuki), John Bocco (Simba), Mzamiru Yassin (Simba), Iddy Nado (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DR Congo). Nickson Kibabage (Difaa El Jadida, Morocco), Said Hamis (Simba) na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (Azam).

BURUNDI

Jonathan Nahimana (Namungo, Tanzania), Philip Nzeyimana (Akademisk BK, Danmark), Youssouf Ndayishimiye (Yeni Malatyaspor, Uturuki), Said Berahino (Zulte Waregem, Ubelgiji), Steve Nzigamasab (Namungo, Tanzania), Fredereric Nsabiyumva (Chippa Utd, Afrika Kusini). Saidi Ntibazonkiza (Sans Club), Blaise Bigirimana (Namungo, Tanzania), Hussein Shabban Shabalala (AS Kigali, Rwanda), Cedric Amissi (Al Taawoun, Arabie Saoudite), Mo Amissi (Heracles Almelo, Uholanzi).

Bonfils Caleb (FK Pohronie,Slovakia), McArthur Arakaza (Sans Club), Ndikumana Trésor (Gasogi Utd, Rwanda), Nimubona Emery Kadogo (Musongati), Ndikumana Asman (Aigle Noirs).Fiston Abdul Razak (ENPPI,Misri), Ndizeye Eric (Musongati), Kaze Gilbert Demunga (Bahache Université de Djibouti), Duhayindavyi Gaël (Mukura Victory Sports, Rwanda)