Stars ni pasi bao

WAKATI Simon Msuva, Nickson Kibabage na Himid Mao wakiwasili leo Oktoba 8 nchini kuungana na wenzao leo, timu ya taifa, Taifa Stars imeanza rasmi mazoezi kujiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa unaotambulika na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) dhidi ya Burundi, huku Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije akionekana akisuka vijana wake kupiga pasi nyingi na kufunga mabao ya kutosha.

Katika mazoezi ya juzi jioni, Etienne alikuwa akiangalia zaidi namna ambavyo timu yake itakuwa ikicheza kwa kuhakikisha kwamba mpira unaanzia kukaa chini ukiwa nyuma na sio kubutua.

Kocha huyo alikuwa akiwajumuisha makipa wake Aishi Manula, Metacha Mnata na David Kissu katika sehemu ya wachezaji wanaoanzisha mashambulizi na sio kubutua mpira mbele, walikuwa wanaanzisha mashambulizi kwa mabeki wa pembeni.

Jambo hili huwa ni tofauti kwani katika mazoezi mengi hata ya Stars yenyewe wakati wakiwa wanajiandaa kufuzu CHAN, makipa walikuwa wanafanya mazoezi ya peke yao hasa yale ya jioni.

Ukija kwa upande wa mbinu, Etienne alikuwa akiwataka viungo wake wanapokuwa na mpira macho yao yaangalie mbele na sio tena kupiga pasi za nyuma kuelekea katika lango lao.

Zoezi hilo lilisimamiwa na makocha wasaidizi, Seleman Matola na Juma Mgunda waliokuwa wamekaa pembeni na kufuatilia kila hatua namna ambavyo wachezaji wao wanafuata maelezo ya kocha mkuu.

Awali zoezi hilo lilionekana gumu, lakini kadri muda ulivyokuwa unaenda wachezaji wao kwa wao walikuwa wakishtuana kama mwenzao alikuwa anataka kupiga pasi ya nyuma na hapo hapo anabadilika na kupiga pasi ya mbele.

Kocha Etienne pia aliwapanga timu mbili wachezaji wake ili aone kama zoezi hilo litaenda vizuri na moja ya timu hizo aliwapanga pamoja kina Manula, Kapombe, ‘Tshabalala’, ‘Sebo’, Mwamnyeto.Mkude, Fei Toto, Ndemla, Sure Boy, Nado na Nchimbi.