TASWIRA YA MLANGABOY : Stars imeaga Afcon ila jamaa wamekamua kinoma!

Muktasari:

  • Farid Musa ameonyesha tofauti ya mchezaji anayecheza daraja la pili Ulaya na yule anayecheza Simba na Yanga au klabu yoyote ya Ligi Kuu Bara.

DAH! Ndio ishakuwa hivyo, hadithi tamu ya kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 imemalizika kwa majonzi makubwa.

Taifa Stars imetolewa katika mashindano ya Afcon ikiwa imeshindwa kuivunja rekodi yake ya mwaka 1980, ambako Tanzania ilifanikiwa kuondoka na pointi moja na mabao matatu katika kundi lake.

Katika Afcon 1980, Taifa Stars katika mechi ya ufunguzi ilifungwa 3-1 na wenyeji Nigeria, mechi ya pili ilifungwa 2-1 na Misri na kumaliza kwa sare ya bao 1-1 na Ivory Coast, katika fainali hizo mabao ya Stars yalifungwa na Juma Mkambi moja na Thuwein Ally aliyefunga mabao mawili.

Miaka 39 baadaye 2019, Tanzania imeanza kwa kufungwa 2-0 na Senegal ikachapwa 3-2 na Kenya nakumaliza kwafungwa na Algeria 3-0, huku mabao yakifungwa na Saimon Msuva na Mbwana Samatta.

Kwangu mimi matokeo haya hayakunishangaza kwa sababu niliona na kama ulifuatilia makala zangu hapa utakubaliana nami.

Pamoja na machungu hayo bado kuna mambo kadhaa nimejifunza na mwenye kutazama mpira kwa jicho la tatu atajua Tanzania tunafeli wapi katika soka la kimataifa.

Sitaki kuwa mnafiki wa nafasi yangu nimefurahi zaidi baada ya Mbwana Samatta na Simon Msuva washambuliaji wetu nyota kufunga japo bao moja moja katika fainali hizi na majina yao yatakumbukwa.

Samatta, Msuva kwa sasa nembo ya Tanzania katika ulimwengu wa soka kwa kile wanachokifanya huko duniani hasa katika klabu zao. Hivyo kufunga kwao dhidi ya Kenya kumefungua milango yao zaidi.

Farid Musa ameonyesha tofauti ya mchezaji anayecheza daraja la pili Ulaya na yule anayecheza Simba na Yanga au klabu yoyote ya Ligi Kuu Bara.

Farid amekuwa katika kiwango bora na uwezo mkubwa wakusaidia timu kufanya mashambulizi kwa kupiga pasi za mwisho za uhakika huwezi kuzungumzia mabao ya Samatta na Msuva bila ya kulitaja jina lake katika kutegeneza nafasi hizo.

Ni matumaini yangu baada ya fainali hizi Farid atapata nafasi ya kuaminika zaidi katika kikosi cha kwanza cha CD Tenerife au kupata klabu nyingine itakayotaka kumsajili barani Ulaya.

Beki Hassan Radhamani Kessy kweli Nkana kumelipa ukiangalia kimo chake na kaumbile kake kadogo unaweza kumdharau ila amepiga mpira wa kazi vibaya mno.

Kessy ameonyesha ukomavu na utimamu wa hali ya juu kile kilio chake cha siku Stars ilipofuzu kwa kuifunga Uganda amekithibitisha kwa vitendo pale Misri.

Changamoto kubwa kwa Kessy ilikuwa mwili wake hasa kimo, lakini uchezaji alitimiza vizuri majukumu yake ametupa sababu nyingine ya kuamiani unapocheza soka la kulipwa nje unakomaa zaidi kuliko ndani.

Mudathir Yahya unaweza kujiuliza anasubiri nini Azam ni wakati wake wa kufungua mkanda na kuondoka nchini akajaribu maisha nje uwezo anao anachotakiwa sasa ni kupata ligi itakayompa changamoto zaidi.

Mudathir alionekana kuchoka na kucheza rafu ambazo hazina msingi, lakini hiyo yote ni kutokana na kutokuwa fiti kwa kiwango cha wapinzani wake wanaocheza katika ligi kubwa za Ulaya.

Kelvin Yondani kweli niamini ukubwa dawa ndicho nilichokiona kwa Yondani alikuwa mtu wa tofauti kabisa. Yondani alicheza kwa kutumia akili na kuwaunganisha vizuri wenzake jambo la kujivunia kwako ni kumaliza fainali hizi akiwa bila ya kadi kitu ambacho wakati mwingine ni ngumu kuamini kama ndiye yeye, lakini yote ni utu zima dawa.

Waswahili wanasema bahati ya mtu ipo mkononi mwa mtu ndio David Mwantika akiwa amerudi Dar es Salaam anapigiwa simu arudi Misri akazibe pengo la Aggrey Morris aliyeumia katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Misri.

Mwantika hakumwangusha kocha wake, Emmanuel Amunike aliyemwita kikosini na kuamua kuanzisha dhidi ya Senegal wengi tulishanga ikiwamo mimi.

Mwantika ametujibu kwa vitendo wale tuliokuwa tunamkosoa na kuwa na hofu na uwezo wake kuna wakati.

Nguvu zake na moyo wake wa kujituma ilikuwa jambo la msingi zaidi katika safu ya ulinzi wa Stars, Mwantika alionyesha umuhimu wa kuwa na mtu wa shoka pale nyuma. Nakuomba radhi Mwantika kwa kutotambua uwezo wako kabla labda kwa sababu Azam hawakupi namba ya kudumu.

Kipa Aishi Manula pamoja na kazi kubwa aliyofanya bado kocha wa kipa wa Simba anatakiwa kumrudisha darasani hasa katika kucheza mipira ya krosi na kuepuka makosa madogo madogo ila kwa ujumla alicheza vizuri. Hakuna ubishi kila mchezaji aliyepewa nafasi Taifa Stars alionyesha uwezo wake na kujitoa ila hawa ndiyo walionikosha zaidi.

Tumemaliza Afcon tuanze maandalizi ya Afcon ijayo hiyo kuanzia kwa klabu, TFF na wachezaji wenyewe watumia mawakala kutafuta timu nje ya nchi ili wakajijenge zaidi huo.

Kadhalika tusisahau kama kuna mechi za kuwania Fainali za Chan 2020 na Tanzania itaanza na Sudan na kama itapenya hapo itavaana na Kenya.