Stand ilipandia mezani na imeshukia mezani

Friday May 31 2019

 

By Charles Abel

WIKIENDI moja ya mwezi Machi, 2014 ilikuwa ngumu sana kwa kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na timu yake aliyokuwa akiinoa ya Mwadui FC.

Licha ya Mwadui kuibuka na ushindi ugenini dhidi ya Polisi Dodoma ambao uliwafanya wawe kileleni mwa moja ya makundi ya Ligi Daraja la Kwanza, walijikuta wakiwa kwenye taharuki kubwa baada ya kukutana na uamuzi tata uliosababisha wakose nafasi ya kupanda.

Uamuzi huo wa machungu kwa Mwadui ulikuwa ni wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuizawadia pointi za mezani Stand United katika siku ya mwisho ya kufunga pazia la Ligi Daraja la Kwanza 2013/2014.

Stand ilipatiwa pointi hizo zilizotokana na rufaa ambayo waliikata kwa Timu ya Kanembwa JKT ya Kigoma kuwa ilichezesha kimakosa baadhi ya wachezaji katika moja ya michezo ya Ligi Daraja la Kwanza baina yao ambayo walipoteza kwa bao 1-0.

Kilichoshangaza wengi hakikuwa ni kitendo cha Stand kupewa pointi hizo tatu za mezani bali kilichoshtua na kuibua mijadala ni muda ambao majibu ya rufaa yalitolewa kwani TFF wakati huo ilikuwa na muda mrefu na wa kutosha kuipitia rufaa ya Stand United lakini ilikuwaje wakangoja hadi siku ya mwisho tena baada ya kuona Mwadui ikiwa na muelekeo mzuri wa kupanda?

Na mwisho wa siku pointi hizo za mezani za siku ya mwisho ziliibeba Stand United kwani ilifikisha jumla ya pointi 32 na kuizidi Mwadui ambayo ilikuwa na alama 31 na kupanda Ligi Kuu lakini iwapo wasingepatiwa, wangebaki na pointi 28 ambazo zisingewapandisha daraja.

Advertisement

Lakini baada ya miaka mitano na miezi miwili, namna na staili ile ile ya kupandia mezani ambayo iliwapandisha daraja Stand United, imegeuka na safari hii ndiyo imetumika kuwashusha kutoka Ligi Kuu kwenda Ligi Daraja la Kwanza.

Baada ya mechi za mwisho za Ligi Kuu licha ya hesabu zote kuonyesha kuwa walipaswa kushuka daraja, walipata miujiza ya kunusurika kwa muda na janga la kushuka baada ya TFF kutoa msimamo wa ligi ambao ulikosewa na kuonyesha kuwa Stand United inapaswa kucheza mchujo na Kagera Sugar ndiyo inapaswa kushuka, lakini baada ya maofisa wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) na Shirikisho hilo kurudi mezani na kupitia upya takwimu za mechi za timu hizo mbili, timu hiyo ya mkoani Shinyanga ikapata kile ambacho imestahili.

Kimsingi inaweza kuwa jambo lisilofurahishwa kwa wakazi wa Shinyanga baada ya kuteremka daraja kwa timu yao pendwa lakini ni jambo ambalo hawapaswi kumtafuta mchawi kwa sababu ni matokeo ya uzembe na makosa waliyofanya wao wenyewe.

Tangu ilipopanda Ligi Kuu, Stand United imekuwa ikikumbwa na migogoro na vurugu za ndani pamoja na mpasuko ambao umesababisha kuwepo kwa makundi mawili ambayo ni lile la Stand Kampuni na Stand Asilia.

Mwanzoni mwa msimu wa 2016/2017 walipata udhamini mnono wa fedha kutoka Kampuni ya uchimbaji ya madini ya Acacia wa kiasi cha fedha kinachotajwa kuvuka Shilingi 2 bilioni kwa mwaka lakini walianzisha mgogoro ambao uliwafanya wadhamini kujiondoa na kujikuta wakirudi kwenye maisha yao ya kubangaiza.

Wachezaji wote muhimu kikosini walifungasha zao virago na kutimkia timu nyingine kusaka malisho mazuri baada ya Stand United kutowalipa stahiki zao kama vile fedha za usajili, mishahara na posho kwa wakati, jambo lililosababisha iwe na kundi kubwa la wachezaji wa daraja la chini ambao wamekuwa hawaleti ushindani kwenye ligi.

Hata hao wachezaji waliobakia kikosini na wale iliowasajili baadaye, hawakuwa wanapata huduma nzuri na kwa wakati, jambo lililopunguza morali yao na kujikuta wakifanya vibaya kwenye ligi. Kabla timu haijashuka daraja msimu huu, ilishakuwa kwenye hatari ya kukumbana na balaa hilo kwenye misimu iliyopita.

Ule umoja na hamasa ya mashabiki wake na wakazi wa Shinyanga vilipotea na kuiacha timu hiyo ikikosa sapoti, jambo ambalo malipo yake yamekuja kuonekana leo hii.

Kushuka kwa Stand United kunapaswa kuwa fundisho kwa timu nyingine ambazo zinapaswa kubadilika na kutafuta namna bora ya kujiendesha ili ziweze kuhimili ushandani wa kwenye ligi badala ya kuigeuza kuwa kijiwe cha kahawa.

Lakini pia kwa wasimamizi wa ligi zetu wanapaswa kuhakikisha tunakuwa na ligi imara ambazo hata kushuka na kupanda daraja kwa timu kutokane na ubora wa timu husika ndani ya uwanja badala ya kutegemea matokeo ya mezani.

Wahenga walisema anayeua kwa upanga naye atakufa kwa upanga. Upanga uleule uliotumika kuwapandisha Stand. leo ndio umewaua kwa kuwashusha.

Advertisement