Stand United yasahau kipigo cha Azam, yaigeukia Singida United

Muktasari:

  • Baada ya Stand United kuchezea kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Azam FC sasa timu hiyo imesema imeelekeza nguvu zake katika mchezo wa keshokutwa Ijumaa dhidi ya Singida United

Mwanza. Stand United ‘Chama la Wana’ imepokea kipondo kizito cha mabao 3-1 kutoka kwa Azam FC katika mchezo wao wa Ligi Kuu Bara, lakini unaambiwa kichapo hicho kimewaumiza na sasa wanajipanga kuhamishia kilio chao kwa Singida United kuhakikisha wanashinda.

Timu hiyo ya mjini Shinyanga katika mchezo wao huo mbele ya Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao, lakini baadaye walijikuta wakisawazishiwa na kudundwa mengine mawili.

Stand United inatarajia kuwafuata Singida United mchezo utakaopigwa kesho Ijumaa kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida ukiwa wa raundi ya 16 kwa timu hizo kusaka pointi tatu muhimu ili kujiweka nafasi nzuri.

Kocha Msaidizi wa Stand United, Athuman Bilali ‘Bilo’ alisema baada ya kupoteza mchezo wao na Azam sasa akili na nguvu zote wanazielekeza katika mechi ijayo dhidi ya Singida United kuhakikisha wanashinda.

Alisema mapungufu ya kiufundi yaliyoonekana katika mchezo uliopita watayafanyia kazi ili kupata ushindi na kujiweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu.

“Matokeo si mazuri, lakini hatukati tamaa kwa sasa tunaenda kujipanga tena na mchezo ujao dhidi ya Singida United kuhakikisha tunashinda na kujiweka katika nafasi nzuri,”alisema Bilo.

Kocha huyo alibainisha kuwa sehemu kubwa watakayoumiza kichwa kufanyia kazi ni safu ya ushambuliaji ambayo itapaswa kutumia nafasi wanazopata na mabeki kuhakikisha wanalinda ushindi.

“Mchezo utakuwa na ushindani kutokana na wapinzani kuwa fiti, lakini tutakachofanya ni kuwaandaa straika wetu kutumia nafasi tutakazopata na mabeki kulinda ushindi,”alisema Bilo.