Staa Aguero pancha tena

MANCHESTER, ENGLAND. MAJANGA yanaendelea kumuandama staa wa Manchester City, Sergio Aguero ambaye alipata majeraha katika mchezo wao uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya West Ham United.

City imeshinda michezo miwili katika michezo mitano ya ufunguzi wa mwanzoni mwa ligi ikiwa inashika nafasi ya 12 kwa alama nane.

Sare hiyo imeifanya kuwa kwenye hali mbaya na hofu imezidi kuwa kubwa baada ya mfungaji wao bora wa muda wote kupata majeraha katika kipindi cha kwanza cha mchezo uliopita na yanaweza kumuweka nje kwa muda mrefu zaidi.

Kocha wa kikosi hicho Pep Guardiola alipoulizwa kuhusiana na suala hilo alisema hajajua itachukua muda gani kupona.

“Alikuwa amepona kabisa kuanzia mchezo na Arsenal na huu, lakini anaonyesha kupata majeraha tofauti na hayo aliyowahi kupata hapo awali. Sijajua itamchukua muda gani. Nafikiri taarifa kamili itatoka baada ya kufanyiwa vipimo,” alisema.

Hii sio mara ya kwanza kwa Aguero kupata majeraha ndani ya mwaka huu. Juni mwaka huu alikumbana na jeraha la goti lililomuweka nje kwa zaidi ya minne, kabla ya kurejea tena mwezi huu na kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Arsenal.

Pep amekuwa na mzimu wa majeraha unaokiandama kikosi chake tangu msimu uliopita ikiwa wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza wana majeraha miongoni mwao ni kiungo wake tegemeo, Kevin De Bruyne, Aymeric Laporte, Fernandinho na Nathan Ake.

“Nilipenda kuwa napata ushindi katika michezo hii mitano hasa mchezo na West Ham lakini imekuwa ni tofauti kwa kuwa wachezaji wangu wengi wamekumbana na majeraha na ratiba inaonekana kuwa ngumu sana hali inayosababisha kutopata muda mrefu wa kujiandaa ukizingatia tunacheza mechi nyingi ngumu kwa kufuatana,” alisema.

“Lakini niwapongeze wachezaji wangu. Wanaonyesha hali ya kujitolea kuhakikisha timu haipotezi na kadri siku zinavyozidi kwenda wanazidi kuwa bora. Kwa sasa nafikiria kuhusiana na mchezo ujao,” aliongeza.

Manchester City mchezo ujao itakuwa ugenini kuumana na Marseille katika muendelezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.