Solskjaer upo? fungate imeisha

 MANCHESTER, ENGLAND. GWIJI wa Manchester United, Roy Keane amemwonya Kocha Ole Gunnar Solskjaer akimwambia kipindi cha kula fungate kimekwisha na sasa anachopaswa ni kuleta mastaa wapya kwenye kikosi hicho.

Keane hafurahishwi kabisa na namna Man United ilivyoanza msimu kwenye Ligi Kuu England na katika mechi ya kwanza tu walichapwa 3-1 na Crystal Palace kabla ya kushinda kwa mbinde 3-2 dhidi ya Brighton.

Katika mechi hiyo ambayo Man United ilishinda, ilikuwa bahati tu kwao baada ya Brighton kugongesha miamba ya goli la wapinzani mara tano.

Keane alisema kuna hofu kubwa sana ameanza kuona kuhusu klabu yake hiyo ya zamani na huenda mambo yakawa mabaya sana kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England msimu huu.

“Fungate imeshaisha kwa Ole, anahitaji kushinda mataji msimu huu,” alisema Keane.

“Hata hivyo, kwa kiwango kile cha wiki iliyopita, presha imeshaanza kupanda.”

Wakati wengi wakiwaonyesha videlo mabeki wa Man United, Keane anaamini kuna wachezaji wengi tu kwenye kikosi hicho cha Old Trafford hawatimizi wajibu wao.

“Ulitegemea kitu fulani kwenye mechi dhidi ya Palace. Kila mtu amekuwa akiizungumzia beki kuwa ni mbovu. Lakini, timu nzima haikuwa nzuri, hasa kwa idadi ya nafasi ambazo walishindwa kuzitumia,” alisema.

Keane anaamini umefika wakati wa Solskjaer kushinda taji la ligi na kumaliza pengo la ubora lililopo baina yao na vigogo Liverpool na Manchester City kwenye ubora.