Solskjaer dili ndio limetiki huko!

Tuesday February 12 2019

 

LONDON,ENGLAND.OLE Gunnar Solskjaer dili limetiki. Hicho ndicho unachoweza kusema baada ya kuripotiwa atachaguliwa kuwa kocha wa kudumu katika kikosi cha Manchester United.

Ripoti zinadai uamuzi huo umeshafikiwa na bodi licha ya kwamba hautatangazwa kwa wakati huo hadi hapo itakapofika mwisho wa msimu.

Man United ilikuwa ikihaha kutafuta mtu wa kuwa kocha wa kudumu kwenye kikosi chao baada ya kumfuta kazi Jose Mourinho na kumpa ajira ya muda Solskjaer.

Lakini, baada ya mechi ya Fulham, ambayo ilishuhudiwa na wamiliki wa klabu hiyo, Joel na Avram Glazer mabosi hao sasa wanaamini mtu sahihi kwenye kikosi chao ni Solskjaer. Avram Glazer alionekana uwanjani Craven Cottage kushuhudia Man United ikiichapa Fulham 3-0 Jumamosi iliyopita.

Alizungumza na Solskjaer baada ya mechi kwenye vyumba vya kubadilisia, huku akiwa tayari alishazungumza na wakala wa kocha huyo, Jim Solbakken, ambaye aliketi pamoja na wakurugenzi hao alipokuwa mgeni mwalikwa wa mabosi wa Man United.

Jambo hilo litazima zile tetesi kwamba Mauricio Pochettino ndiye atakayeenda kuchukua mikoba hiyo ya kuinoa Man United na sasa Real Madrid itakuwa kwenye vita ya peke yao katika kumtaka kocha huyo kama itahitaji kumbadili Santiago Solari mwishoni mwa msimu.

Advertisement

Solskjaer amekuwa na rekodi nzuri huko Man United akiwa hajapoteza mechi yoyote, akishinda 10 katika mechi 11 alizoiongoza timu hiyo kuanzia Desemba na timu sasa ipo kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu England, huku ikiwa pointi tisa nyuma ya Tottenham kwenye nafasi ya tatu na pointi 14 kuzifikia timu vinara Liverpool na Manchester City ambao wanakimbizana vilivyo kwenye msimamo.

Advertisement