Solskjaer aihofia Newcastle

Muktasari:

Timu hizo zimekutana mara 169, Man United imeshinda mara 87, sare 39 na kufungwa 43.

MANCHESTER, ENGLAND. KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amesema mchezo dhidi ya Newcastle United utakuwa mgumu kwa sababu mashabiki wengi wanatamani kuona yeye na wachezaji wake nini watafanya.

Solskjaer ambaye ameanza msimu vibaya akiiongoza Man United kwenye mechi tatu na kushinda moja dhidi ya Brighton amekiri timu yake kutokuwa kwenye kiwango kizuri na akisisitiza watapambana ili kuwapa raha mashabiki wao.

"Nafahamu kwamba, kila mtu ananitazama mimi, kwa sababu ni kocha na hilo siwezi kuliepuka, ikiwa tutapoteza nitakuwa na kesi ya kujibua, lakini kwangu hii sio mara ya kwanza msimu uliopita pia tulicheza mechi nane na kushinda mbili tu za kwanza," alisema.

"Lakini unapokuwa mtumishi wa Manchester United, inahitaji kuwa sawa sawa kiakili na kimwili wakati wowote, hivyo huu ni wakati wa mimi na wachezaji wangu kupigana ili kuwaaminisha mashabiki kwamba tunafaa kuwa  sehemu ya timu hii," aliongeza.

Man United inashika nafasi ya sita ikiwa na imekusanya alama moja tu katika mechi tatu huku mchezo wa mwisho ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza kwa kipigo cha mabao 6-1 kutoka kwa Tottenham Hotspur.

Newcastle nayo inashikilia nafasi ya tisa ikiwa na alama saba baada ya kucheza mechi nne, ikashinda moja, sare moja na ikafungwa mchezo mmoja.

Katika mechi kumi za mwisho Man United imeshinda mara sita ikatoka sare mbili na kufungwa mbili.