Solskjaer adai Bruno ana akili nyingi

Muktasari:

Fernandes amekuwa mkali hata huko alikotokea Sporting Lisbon, ambapo katika nusu ya kwanza ya msimu alifunga mabao 13 na kuasisti mara 10 katika mechi 22 alizocheza kabla ya kunasa dili hilo la kwenda kukipiga Old Trafford.

MARBELLA, HISPANIA . KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amesema kiungo wake mpya Bruno Fernandes ubongo wake unafanya kazi haraka jambo linalowafanya awashinde wanasoka wengi sana duniani.

Staa huyo aliyenaswa na Man United kwenye dirisha la Januari, alicheza mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu England dhidi ya Wolves kabla ya kwenda mapumziko ya baridi huko England.

Fernandes amekuwa mkali hata huko alikotokea Sporting Lisbon, ambapo katika nusu ya kwanza ya msimu alifunga mabao 13 na kuasisti mara 10 katika mechi 22 alizocheza kabla ya kunasa dili hilo la kwenda kukipiga Old Trafford.

Na sasa Kocha Solskjaer amedai kwamba mchezaji wake huyo kwa namna alivyomwona amekuwa na ubongo unaofanyakazi kwa haraka sana na kuelewana na wachezaji wenzake.

“Yote kwa yote, ni mchezaji mzuri sana na ubongo wake unafanya kazi kwa haraka kuliko wanasoka wengine,” alisema Solskjaer.

“Ana mambo mengi sana atakayokwenda kutufanyia. Tutamzoea tu, naye atatuzoea. Pasi zake, anavyogawa mipira, utembeleaji wake wa uwanjani, nafurahishwa na namna ninavyomwona anavyofurahia.

“Anajifua, kujifua na kujifua na kiwango chake cha ubora kipo juu sana, si mchezo.”

Solskjaer amepata nafasi ya kumtazama mchezaji wake mpya kwa karibu zaidi katika kipindi hiki wakiwa kwenye kambi yao huko Hispania wakijiandaa na mchezo mkali dhidi ya Chelsea Jumatatu ijayo uwanjani Stamford Bridge.