Solskjaer,Lampard vikumbo kwa staa wa Pauni 120 milioni

Muktasari:

Man United na Chelsea zote zipo kwenye vita ya kuhakikisha wanamaliza ligi ndani ya Top Four, ambapo kwa sasa kikosi cha Solskjaer kilichopo nafasi ya nane, kimeachwa pointi sita kuifikia Chelsea iliyopo kwenye nafasi ya nne.

LONDON, ENGLAND . JUMATATU kitapigwa kipute cha maana huko Stamford Bridge. Frank Lampard wakati wake sasa wa kulipa kisasi dhidi ya Ole Gunnar Solskjaer.

Mechi ya kwanza wawili hao walipokutana kwenye Ligi Kuu England, Solskjaer alimtandika Lampard 4-0 uwanjani Old Trafford. Sasa marudio ni hapo Jumatatu.

Kocha Solskjaer baada ya kurejea na kikosi chake cha Man United kutoka Marbella, Hispania alikokuwa akikifua kwenye hali ya hewa ya joto, kocha huyo amesema kwamba anaamini timu yake ipo kwenye ubora mkubwa wa kuichapa Chelsea hiyo Jumatatu.

Man United na Chelsea zote zipo kwenye vita ya kuhakikisha wanamaliza ligi ndani ya Top Four, ambapo kwa sasa kikosi cha Solskjaer kilichopo nafasi ya nane, kimeachwa pointi sita kuifikia Chelsea iliyopo kwenye nafasi ya nne.

Wakati wengi wakisubiri vita hiyo ya Ligi Kuu England, Solskjaer na Lampard wamehamishia vita yao kwenye usajili, ambapo kila mmoja akiamini kwamba atashinda kwenye kuinasa saini ya staa Jadon Sancho.

Man United wanajiamini kwamba ni wao watakaoshinda vita hiyo ya kumnasa Sancho, anayedaiwa kuwa na thamani ya Pauni 120 milioni.

Miamba ya soka ya Ujerumani, Borussia Dortmund ipo tayari kufanya biashara ya kumpiga bei mchezaji wao huyo kama kutawekwa mezani ofa ya maana na wanachofurahi ni kuona vita ya klabu za England kwenye kumfukuzia mchezaji wao, kwasababu wanaamini hilo litawasaidia kumuuza kwa pesa ndefu.

Chelsea wanamtaka Sancho, 19, wakimwona kuwa ni mtu anayefaa kutua huko Stamford Bridge kuchukua mikoba ya Pedro na Willian kama wataachana na maisha ya Stamford Bridge mwisho wa msimu huu.

Lakini, Man United wameingia kwenye vita hiyo ya kumrudisha Sancho, England huku wakiamini kwamba kwenye hilo wataweza kuwapiga kikumbo Chelsea baada ya kuonekana kwamba hiyo ni vita ya timu mbili kwenye kufukuzia saini yake.

Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa Man United, Ed Woodward ameshaweka wazi kwamba yupo tayari kutumia pesa nyingi kwenye dirisha lijalo kunasa wachezaji wapya huku wakimweka Sancho kuwa moja ya mastaa wanaohitajika zaidi huko Old Trafford.

Sancho amefunga mabao 12 na kuasisti mara 13 msimu huu na amejitengenezea jina akiwa moja wa makinda wenye vipaji vikubwa huko Ulaya.

Sancho aliibukia kutoka kwenye academia ya Manchester City na kiwango chake huko Dortmund ni balaa huku wakijiandaa kutafuta mtu wa kuja kuchukua mikoba yake atakapoondoka mwisho wa msimu.

Sancho ameshaichezea England mechi 11 kwenye soka la kimataifa, amekuwa Ujerumani kwa miaka mitatu baada ya kusajiliwa kwa Pauni 7.84 milioni tu, huku Dortmund wakijiandaa kupiga faida kubwa kama watamuuza kwa Pauni 120 milioni. Bila shaka, Dortmund hawatakuwa tayari kumuuza kwa ada isiyofikia Pauni 100 milioni.

Ofa ya Chelsea inawapa imani Man United kwamba watashinda vita hiyo na kumnasa Sancho.