Solskjaer, Matic uso kwa uso

Muktasari:

Kiungo wa kimataifa wa Serbia, Nemanja Matic anataka kuzungumza na Kocha Ole Gunnar Solskjaer kuhusu mustakabali wake ndani ya klabu ya Manchester United.

London, England. Nemanja Matic anataka kuzunguma na kocha wake Ole Gunnar Solskjaer, baada ya kupoteza namba Manchester United.

Matic aliyecheza kwa kiwango bora msimu uliopita, amepoteza namba kikosi cha kwanza na nafasi yake inachezwa na kinda, Scott McTominay.

Kinda huyo amempoka namba Matic ambaye tangu kuanza msimu huu hajacheza mechi hata moja.

Matic aliyekuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakitajwa katika nafasi ya unahodha, amepanga kuzungumza na Solskjaer kuhusu nafasi yake Man United.

McTominay anaonekana kutekeleza majukumu yake vyema katika eneo la kiungo mkabaji licha ya Man United kuanza ligi kwa kusuasua.

Solskjaer ametoa nafasi kwa wachezaji chipukizi kucheza nafasi hiyo baada ya kuondoka kwa Marouane Fellaini na Ander Herrera.

Kocha wa zamani wa Man United, Jose Mourinho, alimsajli Matic (31) kwa Pauni40 milioni mwaka 2017 alipokuwa kocha wa Chelsea.

Solskjaer hakuwahi kumpanga kikosi cha kwanza tangu wiki ya kwanza ya mwezi Mei msimu uliopita katika mechi waliofungwa na Huddersfield.

Solskjaer na mchezaji huyo wa kimataifa wa Serbia, watakutana uso kwa uso kuzungumzia mustakabali wake kabla ya dirisha la usajili wa Ulaya kufungwa Septemba 2, mwaka huu.