Solskajaer asubirishwa huko Man United

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa The Mirror, Makamu Mwenyekiti wa Man United, Ed Woodward wamekubaliana na wamiliki wa klabu hiyo mrithi wa Mourinho atatajwa miezi michache ijayo.

MANCHESTER, ENGLAND.MANCHESTER United imechukua uamuzi wa kutoharakisha kumtangaza kocha wa kudumu licha ya Ole Gunnar Solskjaer kuwaacha moto kwenye kikosi hicho kwa sasa.

Man United inaonekana kutulia tangu iwe chini ya Kocha Solskjaer aliyechukua mikoba ya Jose Mourinho baada ya kufutwa kazi huko Old Trafford mwezi uliopita.

Kwa hali ilivyo sasa, Solskjaer ataendelea kushikilia nafasi yake hiyo ya kuwa kocha wa muda hadi mwishoni mwa msimu na baada ya hapo ndipo uongozi wa Man United utakapoamua kumtaja kocha wa kudumu kurithi nafasi ya Mourinho. Kocha huyo, ambaye alikuwa straika wa zamani wa Man United, ameiongoza timu hiyo kushinda mechi zote nane na sasa kelele zimekuwa nyingi zikidai apewe tu kibarua cha kudumu.

Kwa mujibu wa The Mirror, Makamu Mwenyekiti wa Man United, Ed Woodward wamekubaliana na wamiliki wa klabu hiyo mrithi wa Mourinho atatajwa miezi michache ijayo.

Kocha wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino amekuwa akihusishwa sana na kitu hicho tangu alipoondoka Mourinho, lakini Solskjaer amepindua kibao baada ya matokeo ya Ijumaa iliyopita alipoichapa Arsenal 3-1 nyumbani kwao Emirates kwenye Kombe la FA.