Skendo yamng’oa Muthomi FKF

Tuesday July 23 2019

 

By Thomas Matiko

Nairobi. AFISA Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Robert Muthomi hatimaye alizidiwa na presha na kujieungua katika wadhifa wake kufuatia skendo iliyolipuka ikimuhusisha na njama ya kutaka kumuuza mchezaji wa Sofapaka, John Avire kule Misri.

Awali Muthomi alikuwa ameganda kung’oka akisisitiza hajafanya kosa lolote. Hata hivyo, presha kutoka kwa wadau na mashabiki imemlazimu kuondoka ili uchunguzi wa kina uweze kufanywa.

Muthomi alijikuta kwenye mashaka baada ya barua kutoka afisini mwake kuvuja ikiashiria dili chafu ya uhamisho wa straika Avire kutoka Batoto Ba Mungu na kujiunga na klabu moja ya Misri, aliyodaiwa kuwa nyuma ya usukani akisukuma ifanikiwe.

Katika barua hiyo iliyoandikwa Julai 12, 2019 siku 17 baada ya Harambee Stars kubanduliwa nje ya dimba la AFCON, iliomba ubalozi wa Misri kuwasaidia Augustine Ramaita na John Avire kupata visa kwa haraka kuingia nchini humo kama mashabiki ili kutazama mechi za AFCON zilizosalia kutoka Julai 15, 2019 hadi Julai 26, 2019.  Barua hiyo ilitiwa sahihi na Muthomi.

Kilichoibua maswali kibao ni kwa nini Avire alihitaji kupata visa ya kuingia Misri kama shabiki wakati alikuwa mmoja kati ya wachezaji waliounda timu ya Stars iliyokuwa huko kushiriki katika dimba hilo.

Lakini hata zaidi, huyo Avire alihusishwa kwenye mechi mbili dhidi ya Tanzania na Senegal.

Advertisement

Kufuatia ufichuzi huo, Sofapaka iliiandikia barua FKF ikitaka ufafanuzi wa ni kwa nini ilikuwa ikiingilia shughuli za klabu hasa kwenye suala zima la uhamisho wa wachezaji wake. Na hapo ndipo Muthomi alikuwa na kibarua cha kujieleza.

Mara tu baada ya ripoti hizo kulipuka, FKF ilimruka ikitoa taarifa na kusema uchunguzi umeanza na kama akipatikana na hatia, basi itakula kwake.

Awali Muthomi alisisitiza kuwa hatang’atuka katika wadhifa wake, lakini baada ya presha kuzidi, alituma taarifa kwa vyombo vya habari akitangaza kujieungua hadi uchunguzi utakapokamilika.

“Kutokana na mdahalo unaoendelea kufuatia madai ya Sofapaka kuhusu mimi kuhusika katika njama ya uhamisho wa mchezaji wao John Avire, leo asubuhi nimemwomba Rais wa FKF aniruhusu nijiengue hadi uchunguzi utakapokamilika,” taarifa hiyo ilieleza.

Kwa mujibu wa FKF, tayari Muthomi amekiri kusaini barua ile ila kadai hakufanya hivyo akiwa na njama ya kumuuza pasi na ufahamu wa Sofapaka.

Hata hivyo, kulingana na mmiliki wa klabu ya Sofapaka, Elly Kalekwa, Avire na Muthomi walionekana pamoja afisini mwake Alhamisi iliyopita.

“Walikuwa wanafanya nini wakati sisi tunamsubiria arejee kambini? Atamwandikiaje barua ya kumuombea visa wakati ni mchezaji wa klabu yangu na yeye sio afisa hapa,” Kalekwa alihoji.

Advertisement