Siri ya ushindi Simba ipo hapa tu

Muktasari:

Simba iliing'oa Mbabane Swallows na kupata ushindi wa jumla wa mabao 8-1 kisha kuiondoa Nkana Rangers ya Zambia na kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3.

VIJANA wa mjini wanasema lazima mtu apasuke! Leo ndio leo unaambiwa pale Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, patawaka moto na mwisho wa yote ni lazima Mwarabu aache pointi tatu.
Pamoja na JS Saoura iliyotua nchini juzi Alhamisi usiku ikiwa imebeba shehena ya vyakula na maji ya kunywa ikihofia hujuma, lakini Mnyama haachi kitu unaambiwa.
Wawakilishi pekee wa Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba itakipiga na JS Saoura ya Algeria katika mechi ya kwanza ya Kundi D na kuanza safari ya kusaka tiketi  ya kufuzu hatua ya robo fainali.
Wale wazee wa kubeti wapo tayari kupiga mkeka wa maana kutokana nakikosi cha Simba kilivyo kwa sasa wana imani wakiipa ushindi tu, lazima Mhindi apasuke tu.
Simba iliyoanzia hatua mbili za awali ikicheza na Mbabane Swallows na kupata ushindi wa jumla wa mabao 8-1 kisha kuiondoa Nkana Rangers na kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3 kwa mechi zote za nyumbani na ugenini inaaminika itafanya kweli.
Hata hivyo, licha ya Simba kusonga mbele katika hatua ya makundi baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa zaidi ya miaka 15, bado kuna tatizo kwenye baadhi ya maeneo ndani ya kikosi hicho cha Kocha Patrick Aussems.
Benchi la ufundi la Simba linapaswa kuhakikisha linarekebisha makosa ambayo yamekuwa yakifanyika mara kwa mara kwani, kwani yanaweza kuigharimu hasa hatua hii ambayo ni ngumu kutokana na ubora wa wapinzani wao.
Mbali ya kuwa na makosa hayo, lakini kuna mambo ya haraka ambayo lazima yarekebishwe ili kupata ushindi katika mechi ambayo ni muhimu kutokana na kucheza nyumbani.

UMAKINI KATIKA KUFUNGA
Wachezaji wa Simba wamekuwa na makosa binafsi ambayo huwagharimu kwa namna moja ama nyingine katika mechi nne walizocheza hatua za awali kabla ya kutinga makundi.
Safu ya ushambuliaji ya Simba imekuwa ikipoteza nafasi nyingi za kufunga na katika mechi mbili za nyumbani, mashabiki walilalamika baada ya timu yao kushindwa kutumia nafasi hizo.

Dhidi ya Nkana jijini Dar es Salaam ambapo ilishinda mabao 3-1 straika wake, John Bocco alikosa nafasi mbili za kufunga. Ya kwanza alikutana uso kwa uso na kipa Allan Chibwe, baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Claotus Chama lakini mpira wake uliokolewa.
Bocco alikutana tena na mpira akiwa na nyavu lakini alipiga kishuti ambalo lilikwenda kugonga mwamba, hata Emmanuel Okwi naye alikutana uso kwa uso na Chibwe na kufanya kama Bocco tu.
Kama Simba ingeshindwa kupata nafasi ya kusonga mbele, ingezijutia nafasi hizo za wazi ambazo ilishindwa kuzitumia. Katika mchezo wa leo inatakiwa kuwa makini zaidi na kutumia nafasi zote muhimu ambazo itazipata kwa kufunga mabao.

MAKOSA BINAFSI
Makosa ya wachezaji binafsi yamezidi kuonekana kuanzia kwa mastraika hadi mabeki ambao, muda mwingine huifanya timu kuwa hatarini.

Makosa mengine ya Simba yamekuwa upande wa mabeki wake na kipa Aishi Manula.
Mfano katika mechi dhidi ya Nkana  pale Kitwe, Zambia Nicholas Gyan alikokota mpira kwa muda mrefu na kupiga pasi ambayo haikuwa na macho ilinaswa na mchezaji wa Nkana, ambaye alikwenda kufunga bao la kwanza.
Mabeki wa Simba wamekuwa na makosa na muda mwingine kuzozana kama ilivyokuwa katika mechi mbili dhidi ya Nkana.
Katika mechi ya kwanza Gyan alizozana na Wawa, wakati ya pili Wawa alizozana na Aishi Manula mpaka Erasto Nyoni akaingilia kati na kuwaamua.

UKABAJI
Tatizo kubwa ndani ya Simba ni suala zima la ukabaji. Mabeki hufanya makosa mengi na kuigharimu timu. Bao la kwanza kufungwa Simba katika hatua ya awali lilikuwa dhidi ya Mbabane ambalo lilitokana na mpira wa kichwa uliokolewa na beki Gyan, lakini mfungaji alipiga shuti la mbali mbele ya James Kotei na Emmanuel Okwi ambao walishindwa kumdhibiti.
Bao lingine ni dhidi ya Nkana lile la ugenini lilitokana na makosa ya Gyan, ambaye alipoteza mpira na kumuacha Roland Kampamba kutoka nao kati hadi kusogea langoni na kupiga shuti kali ya nje ya boksi.
Bao lingine la Nkana ni lile la katika mechi ya marudiano Uwanja wa Taifa ambapo makosa ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kutokaba kuanzia mbele kumdhibiti winga wa Nkana aliyepiga krosi iliyotua kichwani kwa Walter Bwalya aliyeifungia timu yake bao la kuongoza.

MANULA BADO
Katika mabao matatu ambayo Simba ilifungwa katika mechi nne za mwanzo, mawili yanafanana. Mabao hayo yalikuwa ni mashuti ya mbali yaliyopigwa na timu pinzani na kumshinda kipa Manula.
Mbali ya makosa ya kushindwa kukaba vizuri, bao la kwanza dhidi ya Nkana kule Kitwe na bao la Mbabane yalikuwa ni mashuti ya mbali ambayo yalionyesha udhaifu wa Manula.
Kipa huyo namba moja nchini
anatakiwa kulifanyia kazi hilo ili kuwa bora zaidi.
Siyo katika mechi za kimataifa tu, hata kwenye Ligi Kuu, Manula amekuwa akifungwa mabao ya mbali kama  dhidi ya Alliance, Mwadui na African Lyon.

TIMU ZA KIARABU
Simba inatakiwa kutambua icheza na timu zenye asili ya Kiarabu ambazo zinajua kupoteza muda na kumhadaa mwamuzi kwa kufanya maamuzi, ambayo yanaweza kuwatoa mchezoni.
Kocha Aussems analifahamu hilo kwamba wanakwenda kucheza na timu ya JS Saoura ambayo muda mwingi ikishindwa kupata kile inachohitaji katika mechi hutumia udanganyifu kwa waamuzi.
Kinachotakiwa kwa Kocha Aussems ni kuwaelekeza wachezaji wake wanakwenda kucheza na timu yenye tabia gani ili kujiandaa kiakili na lolote ambalo litatokea waweze kukabiliana nalo.

MASHABIKI WENGI
Wachezaji wa Simba wanaweza kuipigigania timu yao leo dhidi ya JS Soura kutokana na wingi wa mashabiki wao ambao wanajitokeza uwanjani.
Naamini itakuwa ni kama ai zaidi na umati ule ulijitokeza dhidi ya Nkana ambapo Simba ilipata ushindi wa mabao 3-1 na kusonga mbele.
Mzuka huo wa mashabiki wa Simba utawapa mori wachezaji kupambana zaidi ili kupata matokeo bora.
Kocha Aussems katika kutambua mchango huo wa mashabiki amewaomba kujitokeza kwa wingi zaidi ya wale dhidi ya Nkana ili kuwapa nguvu na motisha wachezaji wake kupata ushindi katika mechi hiyo ngumu.