Siri ya rekodi tamu ya Kagera Sugar hii hapa

Muktasari:

Mpaka sasa katika Ligi Kuu ni Azam FC, Kagera Sugar, JKT Tanzania na Yanga ndizo timu pekee hazijapoteza mchezo wowote tangu kuanza kwa ligi hiyo msimu huu.

MWANZA. Kagera Sugar ni miongoni mwa timu nne ambazo hadi sasa hazijapoteza mechi wowote wa Ligi Kuu Bara, lakini nyota wa Klabu hiyo wana siri kubwa juu ya matokeo hayo.

Timu hiyo ya mkoani Kagera imeshuka uwanjani mara tisa na kukusanya pointi 15 na kukaa nafasi ya nane ambapo kati ya mechi hizo imeshinda mitatu na kutoa sare sita.

Wakizungumza baada ya ushindi wa bao 1-0 walioupata jana Jumapili ugenini dhidi ya Lipuli nyota wa timu hiyo walisema kujituma na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ndio siri kubwa ya mafanikio yao.

Mshambuliaji Christopher Edward ‘Edo’ walisema kutokana na muunganiko mzuri walionao wachezaji na morali iliyopo kila mmoja anapambana kuhakikisha anaisaidia timu kupata matokeo mazuri.

Alisema kuwa msimu huu wamejipanga vyema kushinda uwanja wowote na kwamba kiu yao ni kuona wanamaliza mzunguko wa kwanza wakiwa katika nafasi nzuri.

“Kikubwa tunapambana bila kujali tupo ugenini au nyumbani, tunazingatia maelekezo ya Kocha kuhakikisha hatufungwi tumejipanga kumaliza Ligi katika nafasi nzuri,” alisema Edo.

Naye Ramadhan Kapera alisema mwenendo walionao kwa sasa ni wazi watafanya vizuri kutokana na kutambua wanachohitaji na kuwaomba mashabiki kuendelea kuwasapoti.

“Ligi ni ngumu, lakini tunashukuru kwa jinsi tunavyopambana kupata matokeo mazuri tunajitahidi kuendeleza kasi hii hadi mwisho, mashabiki wetu waendelee kutusapoti na sisi hatutawaangusha,” alisema Kapera.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Ally Jangalu alisema msimu huu wamejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri kwao kila mchezo ni kama fainali kushinda au kupata matokeo mazuri.