Singida United yapukutika

Muktasari:

Singida United ni klabu iliyokuwa inaongoza msimu uliopita kuwa na wadhamini wengi kwenye ligi kuu Bara ambapo sasa wadhamini wote wamemaliza mikataba yao na hivyo kukubwa na ukata unasababisha wachezaji kuikimbia timu hiyo yenye masikani yake mjini Singida.

Singida United ipo katika hali mbaya kiuchumi ambayo imesababisha wachezaji kuondoka kikosini huku wachezaji wawili wengine wiki hii wameandika barua za kuachana na timu hiyo.

Wachezaji hao ni Salehe Abdallah ambaye alikuwa akicheza kwa mkopo akitokea Azam FC pamoja na Salum Chuku. Kuondoka kwa wachezaji hao kuimeifanya Singida United ibaki na wachezaji 19 ambao jana Jumatatu walikuwa Bukoba kucheza na Kagera Sugar.

Abdallah alitua Singida United kwa makubaliano ya kucheza lakini tangu afike nafasi yake imekuwa finyu kutokana kwamba nafasi hiyo inachezwa na Elisha Muroiwa raia wa Zimbabwe huku Biniface Maganga naye akisugua benchi katika nafasi hiyo.

Chuku yeye imedaiwa ameandika barua hiyo baada ya kuona maisha ndani ya Singida United yamekuwa magumu ambapo imedaiwa hata mishahara kwao imekuwa migumu huku baadhi wakidai mishahara ya miezi mitano, minne, miatatu na baadhi miwili.

Habari kutoka ndani ya timu hiyo zimesema kuwa wachezaji wanaodai mishahara ya miezi michache ni wale ambao ni mastaa ndani ya timu ambao kwa asilimia kubwa wanategemewa kucheza kikosi cha kwanza.

“Kiukweli maisha yetu ni magumu sana, achana na mambo mengine yanayoendelea lakini hadi ifike wakati wa dirisha dogo pengine watakuwa wameondoka wengi sana, hata mimi nina mpango huo wa kuandika barua ili waniruhusu nikatafute maisha sehemu nyingine,” alisema mchezaji huyo.