Singida United, Sofapaka vitani kwa kocha wa AFC Leopards

Tuesday April 30 2019

 

By Fadhili Athumani

Nairobi. Huenda bingwa mara 13 wa Ligi kuu ya Kenya, AFC Leopards, ikamkosa Kocha wake, Mzambia Andre Casa Mbungo anayepiganiwa na klabu ya Singida United ya Tanzania pamoja na Sofapaka FC, Mwanaspoti imefahamu.

Kwa mujibu wa taarifa nyeti zilizoifikia Mwanaspoti, zinasema kwamba, Ingwe ambayo inashika nafasi ya 10 kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Kenya, inapambana kuhakikisha inambakisha kocha wake huyo, ambaye anamezewa mate kila upande.

Mbungo, aliyejiunga na klabu hiyo, Februari 9, mwaka huu, akirithi mikoba ya Mserbia Marko Vasiljevic, aliyetimuliwa baada ya kusajili matokeo mabaya, ameipandisha Ingwe kutoka mkiani mwa Jedwali hadi nafasi ya 10, jambo lililozivutia Singida na Batoto ba Bamungu.

Mnyarwanda huyo, ambaye sio muongeaji sana, anatajwa kama mmoja wa makocha bora katika ukanda huu wa Afrika mashariki na kati, akiwa na uzoefu wa miaka nane, ya kuundisha soka kwenye ligi kuu ya Rwanda, alikotwaa ubingwa wa Peace Cup mara mbili akiwa na AS Kigali na Police FC.

Rekodi inaonesha kuwa tangu, achukue hatamu pale Ingwe, Mbungo ameiongoza klabu hiyo, aliyoikuta ikiwa katika hatari ya kushuka daraja, kucheza soka safi ya kuvutia, ambapo wamecheza mechi nane za KPL, bila kufungwa.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya AFC Leopards, zinasema kuwa, uongozi wa Singida United, hivi karibuni walifanya mazungumzo na uongozi wa Ingwe, ambapo moja ya Ajenda ilikuwa ni upatikanaji wa kocha huyo, jambo ambalo Leopards, hawako tayari kuona likitokea.

Singida United, inayoshika nafasi ya 11, kwenye msimamo wa ligi kuu ya Tanzania 2018/19, inatafuta kocha mzoefu, atakayerithi mikoba ya Mserbia Dragan Popadic na wanaamini Mbungo ni mtu sahihi wa kunusuru jahazi lao, linaloelekea kuzama.

Aidha, taarifa zinaonesha kuwa Singida kwa sasa ipo katika mikakati ya kujisuka upya, lengo lao likiwa ni kuwa na programu endelevu, ambalo litawasaidia kujiweka pazuri katika harakati za kupigania ufalme nchini Tanzania, ambayo kwa sasa inatawaliwa na SImba, Yanga na Azam.

Wakati hayo yakiendelea kwa upande wa Singida, Rais wa Sofapaka, Elly Kalekwa, alionekana akichati na wawakilishi wa Mbungo, wakati wa mchezo wa Jumapili wa KPL, kati ya AFC Leopards na Bandari, uliofanyika Kenyatta Stadium (Machakos). AFC ilishinda 2-1.

Kalekwa na Mbungo, wanatajwa kuwa na uhusiano wa karibu, kwani ni Mbungo ndiye aliyemshawishi Kalekwa, kumpeleka beki Mnyarwanda, Soter Kayumba, katika klabu ya AFC Leopards, kwa mkopo mapema mwezi uliopita.

Advertisement