Simbu ataka rekodi, medali mbio za Lake Biwa marathon

Muktasari:

Msimu uliopita, Simbu alimaliza wa sita akikimbia kwa saa 2:08:27 ukiwa ni muda wake bora zaidi kulinganisha na ule aliokimbia kwenye mashindano ya dunia ya 2017 wa saa 2:09 na kuwa wa tatu na ule wa Olimpiki ya Rio 2016 nchini Brazil alipotumia 2:11:15 na kumaliza wa tano.

Dar es Salaam.Mbali na kutaka kuiletea Tanzania medali ya tatu ya mbio za kimataifa za Lake Biwa marathoni,  mwanariadha Alphonce Simbu amesema atazitumia mbio hizo kuboresha muda wake kabla ya kwenda kwenye Olimpiki.

Simbu ni miongoni mwa wanariadha nyota wa dunia wa marathoni wanaotarajiwa kuchuana katika mbio hizo za 75 zitakazofanyika Machi 8 mjini Osaka, Japan.

Simbu anatarajiwa kuondoka nchini Machi 5, alisema mbali na kutaka medali ya dhahabu ya mbio hizo, lakini atazitumia kuboresha muda wake na kuweka rekodi ya muda bora zaidi.

Mshindi huyo wa medali ya shaba ya mashindano ya dunia ya 2017, alisema matokeo ya mbio hizo yatampa muongozo na kumpima kikamilifu kuelekea kwenye michezo ya Olimpiki.

"Nahitaji kuweka rekodi nchini Japan kabla ya Olimpiki, mbio za Lake biwa ni fursa tosha kwangu," alisema Simbu.

Mkenya, Wilson Kipsang anashikilia rekodi katika mbio hizo ambayo aliiweka mwaka 2011 alipokimbia kwa saa 2:06:13.

Tanzania ina rekodi ya kutwaa medali mara mbili katika mbio za mwaka 1991 na 2007 zilizochukuliwa na Simon Mrashani aliyekimbia kwa saa 2:11:34 na Samson Ramadhani aliyekimbia kwa saa 2:10:43.