Simbu, Giniki watolea macho Majeshi

Muktasari:

Timu ya riadha ya Ngome  inaundwa na wanariadha wazuri wanaofanya vyema katika timu ya Taifa na mashindano mbalimbali ya kimataifa wakiwemo Magdalena Shauri, Jackline Sakilu, Cecilia Ginoka Simbu, na Giniki.

Wanariadha nyota wa Tanzania Alphonce  Simbu na Emmanuel Giniki wamesema wamejipanga vyema katika mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA).
Wanariadha hao walioko kwenye timu ya riadha ya Ngome  Arusha, waliondoka  jana  kwenda Dar es salaam   kuungana na timu nyingine za majeshi  kabla ya kuanza mashindano Februari 23 hadi Machi 8.
Simbu alisema atashiriki kama sehemu ya mashindano yake makubwa na atatumia nguvu na akili ya ziada kupata mafanikio.
Akizungumza wakati wa mazoezi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jana, kocha wa timu hiyo Anthony Mwingereza, alisema wanariadha hao wako vizuri kutokana na maandalizi ya kutosha waliyofanya.
Mwingereza alisema wanajivunia maandalizi ya muda mrefu waliyopewa na kanda yao, hivyo wanakwenda Dar es Salaam kupambana na si kushiriki mashindano hayo.
Timu ya riadha ya Ngome  inaundwa na wanariadha wazuri wanaofanya vyema katika timu ya Taifa na mashindano mbalimbali ya kimataifa wakiwemo Magdalena Shauri, Jackline Sakilu, Cecilia Ginoka Simbu, na Giniki.
Michezo ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA), ambayo mara ya mwisho ilifanyika mwaka 2004, safari hii inarejea tena kwa kishindo na inatarajiwa kujumuisha wanariadha maarufu wanaotamba katika riadha.