Simbu, Failuna kimeeleweka Olimpiki

Muktasari:

  • Riadha ni mchezo pekee wenye historia ya kuiletea nchi medali mbili za fedha za Olimpiki ambazo zilipatikana kwenye michezo ya 1980 nchini Russia kwenye mbio za mita 5000 na za mita 3000 kuruka vihunzi na kukanyaga maji.

Dar es Salaam. Shirikisho la Riadha la dunia (WA) limewashusha presha wanariadha nyota wa Tanzania wa mbio ndefu za barabarani (marathoni), Alphonce Simbu na Failuna Abdi juu ya hatma yao ya kushiriki Olimpiki msimu ujao.
Simbu na Failuna walikuwa mguu ndani mguu nje juu ya viwango vyao baada ya michezo hiyo iliyokuwa ianze Julai kuahirishwa hadi 2021 kutokana na janga la corona.
Uamuzi wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kuahirisha michezo hiyo uliwaweka gizani wanariadha hao pekee nchini waliokuwa wamefuzu kushiriki Olimpiki kabla ya kuahirishwa endapo wataendelea na viwango vya awali au wataanza upya, huku IOC ikitaka vyama vya kitaifa kuwasiliana na mashirikisho ya michezo yao ya kimataifa ili kujua mchakato wa kufuzu ukoje.
Hata hivyo msimano wa WA,chini ya rais wake, Sebastian Coe umeeleza kuwa wanariadha waliokuwa wamefuzu kabla michezo hiyo haijaahirishwa watashiriki Olimpiki 2021 kule Japan kwa viwango vile vile vya awali.
Makamu wa pili wa rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya ufundi ya RT, Dk Hamad Ndee ameiambia Mwanaspoti Online kuwa WA haijafanya mabadiriko kwa wanariadha waliokuwa wameshafuzu.
"Mpaka sasa tuna uhakika wa tiketi mbili za Olimpiki msimu ujao, lakini wakati wowote mashindano ya kufuzu yatakapoendelea wanariadha wetu wengi watakwenda kutafuta  viwango.
"Msimu ujao tuna plani ya kuwa na timu kubwa ya riadha kwenye Olimpiki, na si timu kubwa, bali itakayorejea na medali," alisema Dk Ndee.
Awali rais wa RT, Anthony Mtaka aliliambia gazeti la Mwananchi kuwa msimu huu watazipa kipaumbele pia mbio fupi na za kati ambazo ndizo ziliwahi kuiwakilisha nchi kwenye Olimpiki ya kwanza Tanzania kushiriki mwaka 1964 wakati huo ikiitwa timu ya Tanganyika, ingawa baadae mbio fupi na za kati zilionekana kupewa kisogo nchini.