Simba yapewa kombe, Sven ageuka bubu

Wednesday July 8 2020

 

By THOMAS NG'ITU

KOCHA mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck amesema ataanza kuipigia hesabu Yanga mara baada ya kurejea Dar.

Akihojiwa na Azam Tv baada ya mchezo dhidi ya Namungo kumalizika, Sven alisema suala la ubingwa kwao wameshafurahia na sasa wanaangalia mambo yanayokuja licha ya kwamba walikuwa katika safari ndefu.

"Tuna mechi na Yanga ndio lakini mipango ya mechi hiyo itaanza baada ya kurejea Dar es Salaam kwa sasa siwezi kuzungumzia lolote," alisema.

Katika mchezo huo uliomalizika kwa sare 0-0, katika kipindi cha kwanza timu zote zilikuwa zikicheza mchezo wa kuviziana

Dakika 9 Namungo walikosa goli baada ya kiungo wake Lucas Kikoti kukiimbia na mpira na alipoingia ndanin ya 18 alipiga shuti dogo lililopanguliwa na kipa Beno Kakolanya na kuuwahi akaudaka.

Dakika 14 Kagere alitumia makosa ya beki wa Namungo ambaye alikosea kukontroo mpira  na ulipodondokea miguuni kwa Kagere hakufanya makosa kabisa na kupiga shuti kali lilipita nje kidogo ya goli.

Advertisement

Viungo wa Simba, Said ndemla, Mzamiru Yassin na Francis Kahata walionekana kutokuwa na mbinu za ziada katika kuwapenya viungo wa Namungo waliokuwa wanaongozwa na Lucas Kikoti.

Dakika 31 Namungo walifanya mabadiliko ya kumtoa Blaise Bigirimana ambaye aligongana na kipa Beno Kakolanya kisha alitolewa na machela na kuingia John Kelvin, mabadiliko haya yaliwanyong'onyesha Namungo kwani nguvu katika eneo la ushambuliaji lilipungua.

Timu zote zilikuwa zikicheza mchezo wa kuviziana kwa kufanya mashambulizi ya kushtukiza katika lango la mwenzake.

Dakika 40 kiungo wa Namungo, Lucas Kikoti alionyeshewa kadi ya njano baada ya kuonyesha ishara ya kukataa maamuzi ya mwamuzi

Abeid Athuman wa Namungo alionyeshewa kadi ya njano baada ya kumpiga kiwiko beki wa Simba, Haruna Shamte.

Namungo katika kipindi cha pili walianza kwa kutaka kupata bao la kuongoza na dakika 46, winga machachari wa Namungo, Abeid Athuman alifyatuka shuti kali na kwenda pembeni kidogo ya goli.

Wakati anapiga shuti hilo aliwatoka mabeki wa Simba, Tairone Santos na Haruna Shamte, wakati huo huo Santos alionyesha kushindwa kuendelea na alitolewa kwa machela na nafasi yake aliingia Gadiel Michael.

Namungo walikuwa wanatumia mawinga wao kuhakikisha kwamba wanaingia safu ya ulinzi ya Simba na walikuwa wanafanikiwa.

Dakika 68 Namungo walikosa goli la wazi baada ya Hashim Manyanya kupiga pasi kwa Lucas Kikoti ambaye aliutuliza mpira kifuani na kupiga danadana tatu na kufytuka shuti ambalo lilipita pembeni kidogo  ya goli.

Kwa upande wa Simba kitendo cha kumuanzisha Meddie Kagere peke yake kilionekana kuwanyima ushindi Simba kwani mabeki wa Namungo walikuwa na kazi nyepesi ya kumzuia mshambuliaji huyo.

Simba walifanya mabadiliko ya kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji kwa kuingia Hassan Dilunga na Deo Kanda na kutoka Haruna Shamte na Francis Kahata na dakika 71 walifanya mabadiliko mengine ya kumtoa Ibrahim Ajibu na kuingia Cyprian Kipenye huku kwa upande wa Namungo aliingia Jamal Issa na kutoka Hashim Manyanya.

Dakika 88 Simba walitaka kupata bao la kuongoza kupitia kwa Meddie Kagere baada ya kupokea pasi ya Shiza Kichuya na kufyatuka shuti kali lakini kipa Nurdin Balora aliudaka moja kwa moja mpira huo.

 

Namungo nao walijibu mashambulizi hayo dakika 89 kupitia kwa John Kelvin ambaye alifyatuka shuti kali la chinichini lakini kipa Beno Kakolanya aliupangua mpira huo na kugonga mwamba kisha beki wa Simba aliuokoa.

REKODI YA SIMBA

Simba wanakuwa mabingwa wa Ligi Kuu mara ya tatu mfululizo huku wakiwa wamechukua mara 21 kihistoria tangu ligi ilipoanza mwaka 1965.

Simba ndio walikuwa wa kwanza kuchukua kombe hili 1965, wakati huo wakiwa wanaitwa Sunderland na walichukua tena mwaka 1966 na 1967 walichukua Cosmopolitans.

Yanga ambao ni watani wa jadi na Simba, wao walishinda kombe hili mara tano mfululizo kuanzia 1968 mpaka 1972 na baada ya hapo Simba walichukua tena mwaka 1973.

Baada ya hapo Simba walichukua taji hilo mara tano mfululizo kuanzia 1975 mpaka 1980 na baadaye walishinda tena mara tatu mfululizo kuanzia 1993 mpaka 1995.

Simba pia walishinda kombe hilo mara nne mfululizoa kuanzia 2001 mpaka 2004 na Yanga waliweza kushinda 2014/2015 na 2016/2017.

Advertisement