Simba yakwepa mtego wa Mazembe

Muktasari:

  • Wachezaji pekee ambao wameonyeshwa idadi kubwa ya kadi zaidi za njano hatua hiyo kwenye kikosi cha Simba ni kiungo Jonas Mkude na beki Murshid Jjuuko ambao hata hivyo, tayari wamekosa mechi wakitumikia adhabu.

KADI ya njano iliyoonyeshwa kwa kipa Aishi Manula kwenye mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita ilianza kuwapa hofu Simba wakihisi kuwa ni ya pili na itamfanya akose mchezo wa kwanza nyumbani wa hatua ya robo fainali dhidi ya TP Mazembe.

Hata hivyo, baada ya kupekua taarifa za michezo iliyopita kabla ya huo ambao Manula alionyeshwa kadi hiyo, imebainika kuwa atakuwepo uwanjani kama kawaida katika mchezo huo wa kwanza utakaochezwa Aprili 6, mwaka huu.

Tangu alipopata kadi hiyo dhidi ya AS Vita ambayo ilitokana na kosa la kuchelewesha muda, vigogo wa Simba walionekana kugawanyika na baadhi walitilia shaka kuwa hiyo ilikuwa ni kadi yake ya pili ambayo inamfanya akose mchezo unaofuata huku wengine wakiamini ana kadi moja tu ya njano akiwemo kocha Patrick Aussems.

Aussems alisema, “Ninadhani Manula ana kadi moja ya njano, nina watu makini walionizunguka ambayo wanafuatilia kwa makini ishu kama hizi.”Lakini, taarifa za mechi sita ambazo Simba imecheza kwenye hatua ya makundi, zinaonyesha Manula ameonyeshwa kadi moja tu ya njano kama ilivyo kwenye hatua ya makundi kama kwa kiungo James Kotei.

Wachezaji pekee ambao wameonyeshwa idadi kubwa ya kadi zaidi za njano hatua hiyo kwenye kikosi cha Simba ni kiungo Jonas Mkude na beki Murshid Jjuuko ambao hata hivyo, tayari wamekosa mechi wakitumikia adhabu.

Lakini, furaha ya Simba imeongezeka zaidi baada ya kufahamu kuwa hata kama Manula na Kotei wakipata kadi za njano kwenye mchezo huo wa kwanza nyumbani dhidi ya Mazembe, watacheza mechi ya marudiano kwani kadi zao walizopata hatua ya makundi zinafutika rasmi kutokana na kuwepo kwa kipengele kwenye kanuni za mashindano hayo kinachoainisha kufutika kwa idadi ya kadi ambazo hazimfanyi mchezaji akose mechi inayofuata.

“Mwishoni mwa mechi za hatua ya makundi, kadi za njano ambazo hazipelekei kukosa mchezo unaofuata, zinafutwa,” kinasema kipengele cha tatu na ibara ya tano ya kanuni za mashindano hayo.

MAKIPA WAMTESA MANULA

Kocha wa makipa wa Mtibwa Sugar, Patrick Mwangata alielezea kiwango cha Manula kipo juu kwa sababu hapati changamoto kutoka kwa makipa wengine hivyo, kuwa midomoni mwa watu pamoja na makocha wake ambao wanakosa chaguo sahihi la pili.

Alisema hiyo ni mbaya kiafya kwani anahitaji mapumziko na kudai kwamba, kujisahau kwa makipa wengine ama kutoaminika na viongozi wao ndiko kunakompa majukumu mengi Manula ndani ya Simba na Taifa Stars.

“Simba wanamtegemea Manula vivo hivyo kwa Taifa Stars, yote haya ni kwa vile hakuna makipa ambao wapo tayari kumpa changamoto Manula, huyu ni binadamu anaweza kupatwa na matatizo muda wowote na timu ikaingia kwenye shida nyingine.

“Dida yupo pale ni mchezaji mzuri, lakini hawajamwani hivyo anajikuta kupoteza utimamu na kujiamini ndiyo maana anashindwa kumpa changamoto Manula, lakini wangemwamini huenda angempunguzia majukumu mwenzake. “Alikuwepo Said Mohamed ‘Nduda’ alikuwepo Simba lakini alishindwa kufanyakazi kama alivyokuwa Mtibwa Sugar, yote hayo ni kutokana na akili zao jinsi wanavyojijengea na kupoteza uaminifu kwa waalimu wao,” alisema Mwangata.

KUBAKI TAIFA

Mashindano yota ambayo yapo chini ya CAF yataendelea kuchezwa uwanja wa Taifa ikiwemo mechi ya Simba na TP Mazembe. Mechi ambazo hazitaruhisiwa kutumia uwanja huo ni zile za Ligi Kuu Bara kwani baada ya mechi ya juzi Jumapili ya Taifa Stars na Uganda uwanja huo utaendelea na ukarabati.

Uwanja wa Taifa unaandaliwa kwa Fainali za Afrika kwa Vijana wa U-17.