Simba yaitangulia Yanga Dar

Muktasari:

Simba imetwaa ubingwa ikiwa na pointi 81 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote huku ikiwa na mechi nne mkononi.

Dar es Salaam. Mamia wa mashabiki wamejitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa ndege wa mwalimu Julius Nyerere kuipokea timu yao ya Simba ambayo imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu bara msimu huu.

Simba jana ilitoka suluhu na Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa Ruangwa mkoani Lindi na baada ya hapo ikakabidhiwa kombe la ubingwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamis Kigwangwalla.

Timu hiyo imerejea leo Julai 9 asubuhi ikiwa na kombe hilo huku mashabiki wakijitokeza kwa wingi uwanja wa ndege kuwalaki wachezaji wao.

Tangu saa 1:00 asubuhi mashabiki walianza kuwasili uwanjani hapo wakiwa katika mabasi aina costa na wengine wakiwa na katika pikipiki zilizofungwa bendera za klabu hiyo.

Simba iliwasili uwanjani hapo saa 2:40 asubuhi na kuendelea kusalia ndani hadi saa 3:18 walipotoka nje na kwenda kwenye gari yao maalum ya wazi iliyopambwa kwa rangi nyekundu.

Kadri muda ulivyokwenda mashabiki walizidi kuongezeka huku baadhi wakiimba nyimbo za kuisifu timu yao.