VIDEO: Simba yafyeka Watano, Sven na Matola nao baibai

Muktasari:

Senzo amesisitiza kwamba hawataki kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi hicho kwani wanataka kuwa na timu imara na ilivyozoweana kama ilivyo sasa.

OFISA Mtendaji mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amethibitisha kwamba kuna uwezekano wa kuachana na mastaa wasiozidi watano hivi karibuni.

Senzo amesisitiza kwamba hawataki kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi hicho kwani wanataka kuwa na timu imara na ilivyozoweana kama ilivyo sasa.

Lakini akaongeza pia kwamba mtihani mkubwa uliopo mbele yao kwa sasa ni kubeba Kombe la FA dhidi ya Namungo, Agosti 2 mkoani Rukwa.

Senzo anasema idadi ya wachezaji ambao Simba inaweza kutangaza kuwaacha msimu huu haitakuwa chini ya watatu au zaidi ya watano.

“Unajua miaka ya nyuma moja ya sababu ambayo Simba ilikuwa ikichangia kushindwa kufanya vizuri walikuwa wanaacha idadi kubwa ya wachezaji mpaka wale ambao ni muhimu, na kila msimu walikuwa wanaanza kujipanga upya kwa kutengeneza timu wakati huo wapinzani wao wanazidi kuimarika.

“Unaweza kukuta mchezaji ambaye anafanya vizuri Simba anaondoka na hata wakati mwingine kwenda kwa wapinzani kuwaimarisha, kwa maana hiyo wakati huu hilo wala halitatokea kwani tumepanga na tumekubaliana kuimarika na kuwa bora zaidi ya kila msimu unaopita,” anasema huku akigoma kutaja majina ya mastaa hao.

Uchunguzi wa Mwanaspoti ndani ya Simba umebaini kwamba Rashid Juma atapelekwa kwa mkopo Namungo FC huku Yusuf Mlipili, Sharaf Shiboub na Tairone Santos ndiyo watakaopigwa chini.

Mlipili na Shiboub ndiyo wachezaji ambao mpaka sasa hawajaongezewa mikataba Simba huku wenzao wakiwa wameshasaini kitambo, lakini Santos ambaye ni Mbrazili amekuwa ni mshangiliaji wa kudumu jukwaani.

Kuhusu kambi ya nje ya nchi, Senzo alisema: “Kama tutapata nchi ambayo haitakuwa na shida ya corona na mazingira ya maandalizi ya msimu yakawa yanaridhisha, tutakwenda huko iwe Afrika au Ulaya, lakini kama itashindikana kabisa hilo, basi tutakuwa hatuna jinsi tutatafuta mkoa wenye mazingira sahihi hapa nyumbani na ndio tutakwenda huko.”

“Tumeanza mipango hii mapema ili kufanya vizuri,” alisema na kuongeza kwamba kwenye usajili mpya ujao hawatazidi wachezaji sita wapya.

Katika hao watatu watatoka nje na wengine wa ndani. Mwanaspoti linajua kwamba Bernard Morrison ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni ambao wameshamalizana na Simba licha ya kwamba wanafanya siri kutokana na utata wake wa kimkataba na Yanga.

Kuhusu usajili wa Ligi ya Mabingwa Afrika, alisema: “Usajili wetu msimu huu utalenga nguvu na ushindani wa kutosha dhidi ya timu za maana ambazo tunakwenda kukutana nazo katika mashindano haya makubwa