Simba ya bilionea

Muktasari:

  • Uongozi mpya wa Simba ambao sasa utakuwa chini ya mfumo wa kampuni ambayo itakuwa na Bodi ya kuisimamia klabu hiyo, umetangaza bajeti ya zaidi ya Shilingi 6 bilioni kwa ajili kugharamia uendeshaji wa shughuli mbalimbali za timu hiyo msimu huu.

HISTORIA mpya imeandikwa ndani ya klabu ya Simba, ndio Simba ile ya zamani sio hii kabisa. Kwa sasa mashabiki wa Simba wana kila sababu ya kutembea kifua mbele na kuwacheka watani wao wa jadi, Yanga kwani wako kisasa zaidi.

Kwa kifupi Simba ya sasa unaweza kuifananisha na klabu zingine kubwa Ulaya kutokana na kuingia kwenye mfumo mpya kabisa wa uendeshaji wake na kuachana na ule wa zamani, ambao migogoro na kulia lia njaa kuliweka mizzi.

Simba hii ambayo itakuwa chini ya mwekezaji, Mohamed Dewji (MO) itakuwa na Mtendaji Mkuu ambaye ni Crescentius Magori na Mwenyekiti wake mpya ambaye ni wa kihistoria Swedi Nkwabi aliyejizolea kura za kutosha na kumfanya kuwa mwenyekiti wa kwanza wa Simba chini ya mfumo mpya wa kampuni.

Uongozi mpya wa Simba ambao sasa utakuwa chini ya mfumo wa kampuni ambayo itakuwa na Bodi ya kuisimamia klabu hiyo, umetangaza bajeti ya zaidi ya Shilingi 6 bilioni kwa ajili kugharamia uendeshaji wa shughuli mbalimbali za timu hiyo msimu huu.

Mhasibu wa klabu hiyo, Amos Gahumeni alisema kiasi hicho cha fedha kitatumika kulipa mishahara na posho kwa wachezaji, benchi la ufundi na watumishi wa klabu hiyo, kulipa gharama za uendeshaji kwa utawala, usafiri, malazi nahuduma nyingine muhimu za timu.

Bajeti hiyo ni ongezeko la zaidi ya Shilingi 2 bilioni kutoka kwenye bajeti ya klabu hiyo msimu uliopita ambayo ilikuwa ni zaidi ya Shilingi 4 bilioni.

Kwa mujibu wa mhasibu huyo, fedha hizo walizotenga kwenye bajeti yao kwenye msimu wa 2019/2018 zitatokana na vyanzo vya mapato vya klabu hiyo ambavyo ni mapato ya milangoni, fedha za haki ya matangazo ya televisheni, fedha za udhamini, ada za wanachama pamoja mauzo ya jezi na vifaa vya timu ambavyo vimekadiriwa kuingiza kiasi cha Sh 4,982, 778,637.

Magori aula

Mkutano huo Mkuu wa klabu ya Simba mbali ya kutangaza bajeti hiyo ya kibabe, jana ulimtaja aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Magori kuwa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu hiyo chini ya mfumo wa uwekezaji wa kampuni ambao ndio unaiendesha klabu hiyo kwa sasa baada ya kufanya mabadiliko ya katiba yake.

Kaimu Rais wa Simba ‘Try Again alimtangaza Magori na kusema ataongoza bodi ya klabu hiyo itakayokuwa na muunganiko wa wajumbe kutoka upande wa klabu ambao ni wawakilishi wa wanachama pamoja na upande wa mwekezaji.

Try Again alimtaka Magori kuhakikisha Simba inatawala kisoka Afrika kama moja ya majukumu yake kwani hivi Sasa klabu hiyo haina tatizo la fedha na kilichobaki mpira uchezwe .

“Hivi Sasa tunakoelekea pesa ipo hivyo uhakikishe Simba inatawala si Tanzania Bali Afrika”alisema Abdallah na wanachama kupiga makofi.

Magori amewahi kuwa Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii(NSSF).

Kilomoni awasapraizi wanachama

Katika hali ya kushangaza, mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Simba, Mzee Hamis Kilomoni jana alitinga kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere ambako kulifanyika Mkutano huo Mkuu wa Simba, na kushangiliwa na umati wa wanachama.

Mzee Kilomoni alikuwa ni miongoni mwa wanachama wa klabu hiyo ambao walikuwa wakipinga mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wake na ilifikia hatua hadi ya kufungua kesi mahakamani.

Kilomoni alisema: “Popote pale Katiba sio msaafu, hii katiba ina mapungufu makubwa sana ambayo yanawanyima nafasi viongozi upande wa klabu na kumpa mamlaka makubwa mwekezaji jambo ambalo si sahihi.

“Tunasubiri watakapoingia ingia madaraka kwamba wataitisha mkutano wa wanachama ili kujadili katiba hiyo,” alisema Kilomoni

Dalali afunguka

Kwa upande wa Dalali alisema, “Kila kitu kimeenda vizuri ingawa kulikuwepo na upungufu kidogo tu upande wa ukumbi, huu ukumbi ni mdogo kwani wanachama ni wengi, Simba hii inapaswa kufanyia mikutano yao kwenye kumbi kubwa zenye uwezo wa kubeba wanachama wengi

“Imedhihirisha kwamba wanachama sasa ni wengi na watazidi kuwa wengi, hivyo tunapaswa kuchukua ukumbi mkubwa, “ alisema na kuongeza

“Lakini wajumbe waliochaguliwa wanatakiwa kufanya marekebisho ya Katiba, hii Katiba ina upungufu mwingi sana, tunatarajia itafanyiwa marekebisho ili itende haki kwa wanachama wake,” alisema Dalali

Umati wafurika mkutanoni

Tofauti na akidi iliyotangazwa awali kuwa mkutano huo utahudhuriwa na wanachama takribani 1,500, jumla ya wanachama 1728 walijitokeza kushiriki mkutano huo hali iliyopelekea kukosekana kwa viti vya kukalia na kusababisha wakae chini kufuatilia mkutano huo.

Pamoja na mshehereshaji (MC) kuwataka wanachama hao kutoziba njia zab ukumbi kwa kukaa chini, wanachama walipaza sauti wakimlalamikia MC kuwa hawana mahali pa kukaa hivyo waachwe wasibughudhiwe.

Ratiba yawachefua wanachama

Kuchelewa kuanza kwa mkutano mkuu wa Simba kuliwakera wanachama wa klabu hiyo ambao walidai ingewabana.

Ratiba ya kufungua mkutano mkuu ilionyesha kuanza saa 3:25 kwa Mwenyekiti kufungua mkutano mkuu ambayo ingefanyika hadi saa 6:30 mchana.

Hadi saa 4:15 asubuhi, mkutano haukuwa umeanza huku baadhi ya wanachama ambao waliomba hifadhi ya majina yao wakilalamika kuwa kuchelewa kuanza kwa mkutano huo kama ratiba ilivyopangwa kutasababisha waburuzwe Katika baadhi ya ajenda hususani ya mapato na matumizi.

“Tuna mikutano miwili, hadi sasa hakuna kinachofanyika, hii si dalili nzuri katika ajenda za mkutano mkuu kwani tuko nyuma ya muda na inaonyesha kuna baadhi ya ajenda hususani ya mapato na matumizi tutaburuzwa,” alisema mmoja wa wajumbe ambaye aliungwa mkono na wenzake ndani ya ukumbini wa JNICC.

Try Again vs HansPoppe

Mkutano mkuu ulichelewa kwa saa 1:24 tofauti na ratiba ilivyoonyesha ambapo Viongozi wa Simba wakiongozwa na kaimu rais, Salim Abdallah ‘Try Again’ aliyeongozana na Zacharia Hanspope na viongozi wengine waliingia ukumbini saa 10:50 Asubuhi na mkutano ukaanza dakika mbili baadae ukifunguliwa na msemaji wa Simba, Haji Manara

Awali, mkutano huo ulipangwa kuanzia saa 3:25 asubuhi.

Vigogo kibao wahudhuria

Mbali na umati mkubwa ya wanachama waliohudhuria, viongozi na wadau wengi maarufu wa klabu hiyo walijitokeza kushiriki kwenye mkutano huo wakiongozwa na Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘TrY Again’, Zacharia Hanspoppe, Juma Kapuya, Hassan Dalali, Mulamu Nghambi, Hassan Hassanoo na wengineo.

Hassanoo asisimua wanachama

Hassan Hassanoo ‘Mpiganaji’ aliamsha shangwe katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere baada ya kutambulishwa. Hassanoo, aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Simba.

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alikuwa akitambulisha watu mbalimbali maarufu na wanachama kupiga makofi lakini alipofika kwa Hassanoo alimtambulisha na kuchombeza kuwa mpiganaji na wanachama walilipuka kwa makofi mengi zaidi.

Kagere atajwa mkutanoni

Mshambuliaji Meddie Kagere ni mchezaji pekee aliyetajwa kwenye mkutano mkuu wa wanachama baada ya Manara kuwaambia wanachama kuwa wachangamke kwani Simba siyo timu ya mchezo mchezo.

“Kagere anawakimbiza tu huko uwanjani, halafu mnakuwaje wanyonge embu changamkeni buana,” alisema Manara huku akikoleza kauli yake kwa kutamka kauli mbiu ya Simbaaa, na wanachama kuitikia kwa nguvu wakishangilia, Nguvu moja.

Ulinzi watawala

Polisi wengi walimwagwa ndani na nje ya ukumbi na mitandao na magazeti yetu ilishuhudia askari hao wa usalama wakirandaranda nje ya Ukumbi huo na wengine ndani wakihakikisha usalama unakuwepo na kuna waliovaa sare na wale waliovaa kiraia.

Askari wengine walionekana kwenye magari yao ya wazi huku wakiwa na silaha na kuimarisha ulinzi kwa kila anayeingia na kutoka katika Ukumbi.

Kauli ya JPM ndani ya mkutano Simba

Kauli ya Rais John Magufuli ilikolezwa kwenye mkutano mkuu huo wa Uchaguzi.

Katika hotuba ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa klabu hiyo, Manara alisema klabu imeagizwa na rais kutwaa ubingwa wa Afrika hivyo kazi ndiyo inaanza.

“Ni klabu moja tu pekee ambayo imeagizwa na rais kuleta ubingwa nayo ni Simba, hivyo kazi ndiyo inaanzia hapa,” alisema Manara huku akishangiliwa kwa nguvu na wanachama.

“Rais Magufuli alitoa tamko la kuitaka Simba itwae ubingwa alipokwenda kwenye mechi ya mwisho ya Ligi kati ya Simba na Kagera Sugar ikiwa ni mara yake ya kwanza kwenda kwenye mechi za Ligi Kuu tangu alipochaguliwa kuwa rais Oktoba 2015,” alisema Manara.

Mishahara ya wachezaji yala 1.4 bilioni

Simba imesema imetumia Sh 1.4 bilioni kulipa mishahara ya wachezaji katika bajeti yao ya mwaka 2017/18.

Akisoma mapato na matumizi ya klabu hiyo ya mwaka 2017/18, mhasibu huyo wa Simba, alisema bajeti yao iliyopita ilikuwa Sh 5.4 bilioni.

Alisema katika bajeti hiyo walitumia sh 1.456 bilion kwenye usajili na Sh1.4 bilioni za mishahara ya wachezaji.

Simba yalipa deni Sh 800 milioni

Try Again aliwaambia wanachama kwamba alipokuwa akikaimu nafasi hiyo aliikuta klabu ikiwa na deni la Sh 800 milioni lililoachwa na viongozi Evans Aveva na aliyekuwa makamu wake Geofrey Nyange Kaburu ambapo, deni hilo limelipwa kwa asilimia 71.5.

“Niseme wazi deni hilo la Sh 800 Milioni chini ya uongozi wangu tumelilipa asilimia 71 na pointi kadhaa na limebaki asilimia 28 na pointi ili kumaliza deni lote.

“Niwahakikishie wapenzi na wanachama wa Simba siku za mbele tutalipa deni hilo na kulimaliza lote.

“Wakati naingia madarakani nilikuta kuna makundi mengi ambayo yalikuwa yakigombana lakini chini yangu nimeyamaliza na hakuna shida yoyote mpaka sasa na ndiyo maana mpira unachezwa Simba, “ alisema Try Again aliyedhaniwa kuwania uongozi.

Imeandikwa na Mwanahiba Richard, Imani Makongoro, Thobias Sebastian, Oliver Albert na Doris Maliyaga.