Simba watamba, tukirudi Dar mtakoma!

Tuesday July 16 2019

 

By Thobias Sebastian na Khatimu Naheka

HABARI ndio hiyo, Simba kwa sasa haipo nchini na iwapo utasikia kuna timu yoyote kuanzia leo Jumatatu inacheza na mabingwa hao wa Tanzania, basi ujue, hiyo ni Simba feki, kwani kikosi hicho kimekula ‘mwewe’ alfajiri ya leo kwenda kambini Afrika Kusini, huku nyota wake wakituma salamu mapema kwa timu pinzani.

Nyota hao wametamba kuwa, wanaenda kunoa makali na wakirejea nchini wiki mbili baadaye ili kuuanza msimu mpya, basi wapinzani wao wakae wakijua hawatakuwa na chao, kwani wamepania kuweka heshima zaidi ya ile iliyowekwa msimu uliopita.

Katika msimu uliopita Simba, ilitetea taji la Ligi Kuu Bara na kubeba Ngao ya Jamii, huku ikifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika sambamba na kucheza fainali za Kombe la Kagame 2018 na Kombe la Mapinduzi na mara zote ikiumia mbele ya Azam FC.

Wakizungumza mapema kabla ya kutimka zao, nyota wapya wa timu hiyo, Beno Kakolanya, Francis Kahata na Wabrazili, Tairone Santos Da Silva na Gerson Fraga Vieira walisema wamepania kwenda kunoa makucha wakijua wana changamoto ndani ya kikosi, lakini pia nje kwenye ushiriki wao wa michuano ambayo timu yao mpya itashiriki 2019-2020.

Kakolanya aliyesajiliwa kutokea Yanga, alisema safari yao ya kuingia kambini anakwenda kupambana kupigania nafasi na jukumu la nani atadaka kati yake na Aishi Manula anamwachia kocha wa timu hiyo, Patrick Aussems.

Kipa huyo alikiri anajua Manula ni kipa mzuri lakini ujio wake ndani ya Simba ni kwenda kutumia ubora wake ambao wekundu hao walioukubali na kuamua kumsajili.

Advertisement

“Najijua, Simba ilivutiwa na ubora wangu ambao niliuonyesha kabla haijanisajili hicho ndicho nitakachokifanya hapa, ubora wangu mkubwa ni kujua kuwapanga mabeki,” alisema Kakolanya aliyesajiliwa Jangwani misimu miwili iliyopita akitokea Prisons Mbeya.

Alisema mbali na kujipanga kuweza kupata nafasi ya kucheza, lakini kiu yake ni kuivusha Simba mahali ilipokuwepo kwa msimu uliopita akishirikiana na wenzake, huku akitamba wapinzani wao kwenye michuano yote itakayocheza Simba, lazima wajipange kwelikweli.

“Ninapokuwa langoni naona timu nzima najua nizungumze nini kabla ya shambulizi halijafika golini hicho huwa kinanisaidia sana, nakwenda kujiandaa kupigania nafasi.”

Naye Santos Da Silva mwenye urefu wa mita 1.91 alisema urefu wake umekuwa silaha kubwa katika kubalina na mipira ya juu iwe katika kuzuia na hata kufunga anapopanda kuongeza nguvu.

“Unaponiona na huu urefu wangu, jua ni kitu kinachonisaidia kukabiliana na mipira ya juu vyema kwa kuhakikisha nashinda kupiga kwa kuokoa na hata ninapopandisha mashambulizi pia naweza kufunga,” alisema Tairone.

Tairone alisema ubora wake mkubwa wa kukabiliana na mipira ya juu na kucheza kwa hesabu ndiyo kitu anachotaka kukiongeza katika ujio wake ndani ya klabu hiyo na licha ya ugeni wake Msimbazi, lakini amekuja kuongeza kitu katika mafanikio.

Mbrazili mwingine, beki Gerson Fraga Vieira alisema hana wasiwasi juu ya ubora wake na umoja wao na mabeki atakaocheza nao na anataka kujituma kuhakikisha Simba inakuwa na ukuta mgumu utakaowapa matokeo mazuri.

“Malengo yangu kama beki ni kuwa na umoja na wenzangu ambao tutakuwa nao, kama beki najua majukumu yangu vyema, Simba imekuwa ni klabu ya mafanikio hilo tunatakiwa kuliendeleza kwa muda nitakaokuwa hapa,” alisema Vieira ambaye ni beki wa kati pia.

Kiungio fundi wa mpira kutoka Kenya, Francis Kahata alisema malengo ya klabu pamoja na kikosi bora ndiyo vitu vilimfanya ajiunge na timu hiyo na sasa anakwenda kujiandaa kuhakikisha anakuwa sehemu ya kikosi cha kwanza.

“Nina uwezo wa kucheza nafasi kama mbili au tatu uwanjani ni uamuzi na kujituma kwangu ndio kutamshawishi kocha, nimefurahi kuwa sehemu ya kikosi cha Simba, timu inayoonyesha ina malengo makubwa,” alisema Kahata aliyetua Simba akitokea Gor Mahia

WAPIGWA MSASA

Nyota wote wa Simba na benchi lao, jana Jumapili walipigwa msasa na wadhamini wakuu wa klabu hiyo, huku wakipiga msosi wa nguvu ikiwa ni mwanzo wa safari mpya ya msimu mpya. Semina hiyo ilifanyika mchana wa jana kabla ya jioni wachezaji kupaki mabegi yao kuwahi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JKN kuanza safari yao ya kwenda Afrika Kusini wakitarajia kuweka kambi jijini Johannesburg.

MSIKIE MAGORI

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori aliliambia Mwanaspoti jumla ya wachezaji 27 na watu wa benchi la ufundi wanane wakiongozwa na Kocha Aussems wapo kwenye msafara huo na kusisitiza kambi wanayoenda ni bab’ kubwa kwa wachezaji wao.

Magori alisema kambi hiyo ni rafiki na itakayowapa utulivu wachezaji wa kuweza kuelewa kila kitu wanachopewa na makocha wao na kuwataka wanaondoka kwenye benchi la ufundi ni makocha Aussems na wasaidizi wake Denis Kitambi, Zrane Adel, Muharami Mohammed ‘Shilton’, Meneja Patrick Rweyemamu, Mtunza Vifaa, Hamis Mtambo na Mratibu Ally Abbas Suleiman.

“Wachezaji wote waliosajiliwa wakiwamo wapya na wale waliokuwepo msimu uliopita wataondoka wote na kama tutakamilisha usajili ya mchezaji mwingine wa mwisho, basi ataungana na wenzake kwani hatujafunga usajili,” alisema Magori.

Nyota 27 waliosajiliwa Simba ni pamoja na Aishi Manula, Kakolanya na Ally Salum, huku mabeki wakiwa ni Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Gerson Vieira, Shomary Kapombe, Kennedy Juma, Yusuf Mlipili, Paul Bubaka, Gadiel Michael, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Tairone Santos Da Silva.

Wengine ni Francis Kahata, Jonas Mkude, Sharaf Eldin Shiboub, Juma Rashid, Hassan Dilunga, Mzamiru Yasin, Said Ndemla na Clatous Chama ambao ni viungo.

Safu ya ushambuliaji ya Simba ina wakali wafuatao Ibrahim Ajibu aliyetokea Yanga, John Bocco, Miraj Athuman, Meddie Kagere, Deo Kanda na Wilker Henriques da Silva.

Advertisement