Simba walivyoibeba Namungo

Wednesday September 30 2020
simba pic

PAMOJA na Kocha wa Namungo, Hitimana Thierry kukaririwa akisema asilimia kubwa ya usajili uliofanywa msimu huu hayakuwa matakwa yake, wapo wachezaji ambao kwa uzoefu wao wanaweza wakasaidia timu hiyo kwenye, Kombe la Shirikisho Afrika.

Msimu uliopita Thierry alikuwa na kikosi kizuri kilichoisaidia timu hiyo, kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, akiwemo Reliants Lusajo aliyemaliza na mabao 13 na sasa kahamia (KMC), LucaS Kikoti na Bigirimana Blaise hao bado wapo.

Katika usajili wa msimu huu kuna mastaa wapya ambao wamekwenda kuongeza nguvu ndani ya kikosi hicho na wana uzoefu wa kucheza michuano ya kimataifa na ligi ya ndani, hivyo uwepo wao utaibeba timu hiyo.

HARUNA SHAMTE

Alitamba akiwa na Simba kwa misimu mitatu mwaka 2011 mpaka 2014, kabla ya kwenda JKT Ruvu, kisha Mbeya City na Lipuli.

Simba ilimsajili tena msimu uliopita kwa mwaka mmoja kabla ya kuvunja mkataba wake kutokana na kukosa nafasi mbele ya Shomary Kapombe na sasa amejiunga na Namungo kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Advertisement

Kutokana na uzoefu wake Ligi Kuu na michuano ya kimataifa, Shamte anaonekana kuwa msaada ndani ya kikosi hicho, kinachotarajia kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.

MIZA BALE

Alianza kikosi cha vijana cha Simba kilichokuwa kimesheheni nyota kama, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla, Jonas Mkude, Abdallah Sesema, Ramadhani Singano ‘Messi’ na wengineo wengi.

Hakufanikiwa kucheza timu ya wakubwa licha ya kuwa nahodha kwenye kikosi cha vijana , huku akipita kwenye timu mbalimbali za madaraja ya chini wakati huo, kama Namungo aliyofanikiwa kuipandisha daraja na amekuwa nayo mpaka sasa.

Uwepo wake ndani ya timu hiyo unatazamwa kama msaada kwenye michuano mbalimbali.

CARLOS PROTAS

Kama Miza Bale, alianzia kikosi cha vijana Simba lakini alishindwa kucheza timu ya wakubwa.

Protas aliamua kwenda kusaka changamoto kwengineko na alizichezea Toto Africans na huko alikuwa beki kisiki na tegemeo. na hivyo Namungo ilimwona na kumtumia ikiwa Daraja La Kwanza na mpaka sasa anatumika kama mchezaji wa kikosi cha kwanza akiwa tegemeo licha ya msimu huu kutokuanza vizuri ligi kutokana na majeraha.

ABDULHALIM HUMUD

Amecheza ligi mbalimbali nje ya Tanzania kama Afrika Kusini na Uarabuni. Pia hapa nyumbani amezichezea Ashanti United, Mtibwa Sugar KMC, Azam FC na Simba.

Humud ambaye msimu huu amesajiliwa kwa mkataba wa mwaka mmoja na Namungo ni mmoja wa nyota waliowahi kupita Simba mwaka 2011 na kucheza kwa mafanikio na alijiunga pia na Azam mwaka 2014 na uzoefu wake unatazamia kuja kuibeba Namungo kwenye michuano ya kimataifa.

SHIZA KICHUYA

Kichuya kona.... bao. Ndio bao lililompa umaarufu akiwa Simba kabla ya kutimkia Misri kukipiga soka la kulipwa kwenye klabu ya NPPI.

Msimu uliopita alirejea Simba kwa miazi sita baada ya kushindwa soka la Misri na msimu huu ametua Namungo na huko ameonekana ataisaidia pakubwa kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mbali na Simba akicheza nayo pia michuano ya kimataifa, ameichezea pia Taifa Stars na hilo tu linambeba kuisaidia Namungo.

ADAM SALAMBA

Mwaka 2018, Simba ilimsajili straika huyo kutoka Lipuli kwa mkataba wa miaka miwili ambayo hakufanikiwa kuimaliza kwani alitumika kwa msimu mmoja tu, ikamtoa kwa mkopo kwenda Namungo, hata hivyo milango ya bahati ilikuwa wazi kwake akapata timu nchini Kuwait ya Al Jahra FC.

Kilichomrejesha kucheza Ligi Kuu Bara ni baada ya nchi ya Kuwait kuwa na changamoto wa ugonjwa wa covid 19, hivyo walivunjiwa mikataba wachezaji wote wa kigeni, uwepo wake Namungo utakuwa na faida kuisaidia kimataifa.

KELVIN YONDANI

Mwanaspoti lilikufichulia usajili wa Yondani aliyejiunga na Namungo kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Yanga, alikotumika miaka nane.

Uwepo wake ndani ya kikosi hicho, kuna manufaa kwani ni beki mzoefu na michuano ya kimataifa na ligi, lakini changamoto ambayo kocha wake anatakiwa kumjenga ni kuepuka rafu ambazo zinaweza zikawa zinaigharimu timu yake.

Ni mchezaji ambaye amezitumikia klabu kongwe kwa nyakati tofauti kwani alijiunga na Yanga msimu wa 2012/2020 akitokea Simba ambako alicheza msimu wa 2006/12.

JAMAL MWAMBELEKO

Alianzia timu ya vijana ya Simba na hakufanikiwa kupandishwa timu ya wakubwa, kabla ya kuamua kwenda kucheza soka kwengineko mwaka 2017.

Mwaka 2017, aliichezea Mbao FC na kufanikiwa kuwa moja ya mabeki waliofanya vizuri na kuwavutia Simba ambao walimsajili kwa miaka miwili.

Hakufanikiwa kucheza mara kwa mara.

Alivunja mkataba na kujiunga na Singida na hakukaa sana alienda kucheza soka la kulipwa Kenya kwa mwa mmoja.

Mwambeleko alirudi nchini na Januari mwaka huu, katika dirisha dogo alisajiliwa na Namungo kwa mkataba wa mwaka mmoja, timu hiyo itafaidika na mchezaji huyo kutokana na uzoefu wake kimataifa na ligi ya ndani.

 

Advertisement