Simba pasi 552, Xavi Hernandez pekee pasi 859

SIMBA walinawiri juzi katika uwanja wa taifa, hasa mchezaji aliyeitwa Clatous Chota Chama. Mtaalamu wangu wa takwimu, Anwar Binde alikuja na takwimu zake mwisho wa mechi. Simba walipiga pasi 552 katika pambano hilo.

Namuamini Anwar kwa sababu amesomea kazi hiyo Uganda. Simba ilitawala mechi nzima huku Chama akipiga pasi zaidi ya 60. Simba inacheza katika sayari yake hapa nchini. Kuna Simba halafu kuna timu nyingine. Haishangazi kuona imechukua ubingwa wa Bara mara tatu mfululizo.

Wakati fulani unawatazama wachezaji wa Simba na kujiuliza kwanini wameshindwa kucheza soka la juu zaidi ya hapo. Labda wangeweza kwenda mbali zaidi na kucheza katika klabu mbalimbali kubwa na ndogo barani Ulaya.

Hapohapo nikarudi nyuma kupekua mafaili. Nikakumbuka jinsi ambavyo mchezo wa soka una viwango vyake. Waingereza wanasema “standard”. Nimegundua tuna kazi kubwa ya kumuandaa mwanasoka wetu afikie viwango vya kimataifa.

Wakati huu tunajiuliza nini kinaendelea kwa Mbwana Samatta pale Aston Villa. Ameshindwa kufikia viwango vyao? Hapohapo tunajiuliza, kwanini wanasoka wetu hawachezi nje ya nchi kwa wingi. Kuna viwango ambavyo wenzetu wameweka na vinaogofya. Katika pambano la juzi Simba walipiga pasi hizo na kung’ara mno. Katika pambano la michuano ya Euro mwaka 2012 kati ya Hispania na Ireland, kiungo mahiri wa zamani wa Barcelona, Xavi Hernandez akiwa na jezi ya Hispania alipiga pasi 859.

Hii ina maana kwamba Xavi peke yake alipiga pasi nyingi zaidi akikaribia mara mbili ambazo kikosi kizima cha Simba kilipiga juzi. Unajiuliza Xavi alikuwa mwanadamu au mashine? Kabla haujawaza sana unajiuliza kiwango ambacho mwanadamu mmoja anafikia kuwa fiti na makini kiasi hiki.

Baada ya hapo unajikumbusha kwamba tunahitaji wanasoka wetu wengi waende kucheza na kutamba La Liga na kwingineko. Sawa, Xavi ni alama ya pasi duniani. Alikuja kubadilisha soka kutoka katika mbwembwe za kina Ronaldinho na kwenda katika pasi. Hata hivyo, haibadilishi ukweli kwamba kuifanya kazi hii kwa ufasaha kunatukumbusha mengi. Kama Simba ni bora kiasi hiki, na wote tunaikubali kiasi kikubwa, mimi nikiwa shabiki wao mkubwa wa staili yao ya soka, inakuaje wanazidiwa kiwango cha pasi zao zote na mchezaji mmoja.

Hapa tunawakumbusha wachezaji wetu wajiandae hasa kama wanataka kucheza soka Ulaya. Sio lelemama. Na vilevile tuache kuwatukuza wachezaji na kuwafananisha na baadhi ya mastaa wanaocheza Ulaya. Kumbe wale wanacheza katika viwango tofauti na sisi. Haijalishi kama ni mchezaji wa kawaida au wa ajabu. Kuna watu wengi wanaombeza Samatta kwa kumlinganisha na baadhi ya mastaa wanaotamba katika Ligi Kuu Bara. Utasikia tu mtu anarokopoka “Ajibu ni bora kuliko Samatta.” Unatumiaje kumlinganisha mchezaji wa Ligi Kuu England na huyu wa Ligi Kuu Bara? Tujifunze yafuatayo. Kwanza, tutengeneze makinda ambao wataenda Ulaya wakiwa na umri mdogo. Walau watajitahidi kuingia katika mifumo ya kule na kujua kinachohitajika katika kupiga pasi 859 ndani ya mechi moja. Sio kitu cha kawaida. Hauwezi kwenda Ulaya ukiwa na miaka 23 halafu ukategemea kufanya maajabu.

Tuelewe pia umuhimu wa kuwa na shule za soka za watoto zenye ubora wa kumfanya mchezaji awe na utimamu wa mwili. Bado tunajali sana kipaji kuliko utimamu wa mwili wa mchezaji kuanzia ngazi ya chini hadi ile ya juu. Hapo hapo tujifunze kuweka akiba ya maneno. Tusiwasakame sana baadhi ya wachezaji wanaorudi nchini na kushindwa kufikia malengo ambayo walijiwekea au sisi wenyewe tuliwawekea wakati wanaondoka. Kwa mfano, binafsi nilikuwa na matumaini makubwa na Farid Mussa alipoondoka nchini kwenda kucheza soka la kulipwa katika klabu ya daraja la kwanza ya Tennerife pale Hispania. Niliamini kwamba Farid angefika mbali.

Ni kweli Farid alikomaa Ulaya. Amepambana kwa miaka mingi mpaka alipoamua kurudi. Halikuwa suala la miaka miwili. Ilikuwa zaidi ya hapo. Unapopitia mifano kama hii ya Xavi na Simba unajifunza kuwa mpira una viwango tofauti vilivyopitiliza. Mchezaji anayefunga mabao 10 Ulaya ni sawa na mchezaji anayefunga mabao 30 katika ligi yetu. Haishangazi kuona mchezaji wa Celtic anayefunga mabao 57 pale Scotland hawezi kuingizwa kuwania kiatu cha dhahabu dhidi ya Lionel Messi atakayefunga mabao 40 kwa msimu. Wanajua Messi amefunga mabao yake katika Ligi Kuu ya Hispania au katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Mechi ambazo zipo katika kiwango kikubwa zaidi kuliko mfungaji bora wa Scotland. Viwango ni tofauti kwa kiasi kikubwa.

Wakati fulani unaudanganya moyo wako kwamba Chama wa Simba anaweza kutamba Ulaya. Hapohapo unawekewa takwimu mezani. Katika pambano la juzi, Chama hakufikisha pasi 70 licha ya kuwa mchezaji bora wa mechi. Juzi hiyohiyo Thiago Alcantara aliingia katika pambano la Chelsea akiwa na jezi ya Liverpool na kupiga pasi 75. Alizipiga kwa dakika 45 tu. Unawaza Thiago ana kifua gani au yuko fiti kwa kiasi gani. Anayafanya haya katika mechi ya kiwango cha juu kama hii ya Chelsea dhidi ya Liverpool Stamford Bridge na sio dhidi ya Biashara Mara. Mpira sio lelemama sana.