Simba inapovuna mafanikio ya utulivu wa uongozi

Muktasari:

Simba wamekuwa na utulivu kuliko kuvurugana wala hakuna mabishano makubwa na hata kama yakiwepo basi ni ndani ya klabu ambayo ni wa kawaida kwa watu kutofautiana

Simba imechukua mataji yote ya ndani kuanzia ngao ya hisani, wakachukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao kwao wanachukua kwa mara ya tatu mfululizo na sasa wamemalizia na taji la Kombe la Shirikisho.

Hakuna medali ambayo Simba imeiacha labda iwe ya mshindi wa pili, lakini kwa kuwa bingwa kote wamechukua kwa kishindo wakionyesha ukomavu mkubwa mpaka wanapata mafanikio hayo ya ndani. Huu ndio ukweli.

Wengi ambao ni mashabiki wa timu hiyo wanaona wazi walistahili mafanikio, lakini pia wapo ambao hata ukiwawekea kisu shingoni hawatakubaliana na mafanikio hayo ya Simba.

Kwenye kundi hilohilo wapo pia ambao watakubaliana na ukweli wa ubora wa Simba, ingawa watakuwa wagumu kusema hadharani na mwisho ambao watakuwa hawajui lolote nao wapo, usibishe.

Simba kupata mafanikio hayo yapo mengi ambayo yamewawezesha kufikia hatua hiyo - kubwa lazima utambue utulivu walioutengeneza katika klabu yao kwa ujumla wakifanya mambo yao kwa utulivu mkubwa.

Tuliza akili yako kisha fikiria jinsi uongozi wa klabu hiyo ulivyotulia ukifanya mambo yao kwa akili kubwa.

Wamekuwa na utulivu kuliko kuvurugana wala hakuna mabishano makubwa na hata kama yakiwepo, basi ni ndani ya klabu ambayo ni ya kawaida kwa watu kutofautiana.

Tangu kujiengua kwa aliyekuwa rais wao, Swedi Mkwabi hatua ambayo ilishtua kwa kiasi fulani, lakini Simba ilionekana kutulia na kufanikiwa kutuliza presha na mambo kuendelea chini ya bodi yao ya wakurugenzi inayoongozwa na Mohamed Dewji ‘MO’.

Ukitoka hapo, sekretarieti yao nayo chini ya mtendaji mkuu, Senzo Mazingisa unaweza kusema hawapo, lakini wapo, kwa kufanya majukumu yao hakukuwa na vurugu zozote.

Kila kitu kilionekana kupita katika njia yake na kuondoa dosari katika maeneo mengi.

Toka hapo, shuka katika benchi lao la ufundi na hata kikosi chao.

Kwa ukamilifu nako kuna wakati upepo mbaya unavuma, lakini kutokana na uimara wa walio juu yao kila kitu kitulia na safari yao kuendelea kama ambavyo wanataka.

Utulivu wa maeneo yote huko juu ukawafanya wanachama na mashabiki nao jukumu lao kuwa moja tu, kushangilia timu yao.

Katika hilo hawakuwa na presha kubwa sana kwa uongozi wao hata pale walipokuwa wakali walipo na mambo hayajatulia, lakini walio juu yao walikaa sawa na kuwafahamisha yanayoendelea kwa kufanya maamuzi na baadaye mambo kutulia, na safari ikaendelea.

Nidhamu hii klabu nyingi zinaikosa.

Klabu hizo wanataka mafanikio wakati ukiangalia uongozi wao wa juu mpaka benchi lao la ufundi hakujatulia. Kila kitu kinakuwa kinaendeshwa kwa vurugu kuliko ubora wa uongozi. Huwezi kupata mafanikio.

Huko nyuma Simba waliishi maisha yao. Vuta picha wakati wanavunja viti uwanjani, lakini baadaye walifikia hatua ya kutimuana viongozi kwa viongozi kisha baadaye ikaja hali mpaka ya kutimua wachezaji.

Hapana shaka katika kipindi hivho walijifunza na kuamua kutoka hapo walipo.

Haitakuwa dhambi na klabu zingine nazo kuangalia upya aina ya maisha wanayoishi kwa kuthubutu hata kuwaangalia Simba wanavyoishi kama kweli wana nia ya kutaka mafanikio, kwani siku zote kupanga ni kuchagua - kipi unataka ukivune katika kilimo chako.

Inawezekana zipo klabu huko nyuma zilipata mafanikio makubwa na kuishi maisha ambayo Simba inaishi sasa, lakini wanapaswa kujiuliza waliwezaje kufanikiwa nyakati hizo na sasa kipi kinawashinda, kisha tathmini hiyo itawasaidia katika kubadilika.

Simba inafundisha mengi kama sio kukumbusha jinsi mtu au taasisi anavyotakiwa kuishi kwa kujipanga, kisha baadaye uanze kuvuna matunda ya ubora wako uliojitengenezea mwenyewe.

Kwa sasa klabu mbalimbali zipo katika nyakati za kuboresha vikosi vyao. Hapa kila mtu ataangalia aliteleza wapi. Niwakumbushe jambo moja, wakimaliza kuchukua wanachotaka ili wapate mafanikio pia waangalie aina ya uongozi wao na wanaishi maisha ya aina gani. Wakijua wanakosea wapi watabadilika, lakini kama hawatajua wapi wanateleza anguko litazidi kuwa kubwa kwao. Hongereni Simba wengine igeni sio dhambi.