TASWIRA YA MLANGABOY : Simba imebutua, Yanga, Azam msishangae CAF

Saturday June 8 2019

 

By Andrew Kingamkono

USHAWAHI kucheza kombolela wewe?! Kama ndio najua unafahamu pale mtu wa mwisho anapoambiwa uma kidole cha mwisho akisubiriwa aje kuwakomboa wengine kwa kulipiga kopo au mpira.

Najua watoto na vijana wengi wa leo hawaujui mchezo huu wa kombolela, wao wamezoea kucheza play station na kuangalia katuni pamoja na kufanya homework nyingi kila ifikapo jioni.

Pia, bila ya kusahau kuwa, kwa sasa watoto wengi wanakaa geti kali ikifika saa 12 jioni wote ndani hakuna sehemu ya kucheza michezo ya kujificha ya usiku kama tulivyokuwa tunacheza enzi zetu za kombolela mchezo pendwa zaidi.

Taswira imeanza na hadithi ya kombolela kwa sababu ya tukio lililotokea Jumanne hii baada ya Ofisa Habari wa Shirikisho Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo ikieleza Tanzania imejiongezea nafasi ya kupeleka timu zake katika Mashindano ya Afrika baada ya Tanzania kuwa katika nafasi 12 bora kwenye viwango vya CAF.

Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu zilizofanyiwa marekebisho na kamati ya Utendaji baada ya kupatikana nafasi nne (4) timu za Tanzania zitakazowakilisha kwenye mashindano hayo ni Simba, Yanga Ligi ya Mabingwa (CAF CL), Azam FC na KMC zenyewe Kombe la Shirikisho (CAF CC).

Nilipata tabu kuamini nilichokiona kwanza nilijua kanuni hiyo itaanza kufanya kazi msimu 2020/21 mbona ghafla imerudi nyuma na kuanza msimu ujao 2019/20.

Advertisement

Pili lililonifanya niwe mgumu kuamini ni rekodi ya hivi karibuni ya rafiki yangu Ndimbo katika taarifa zake ukizingatia alishusha Kagera Sugar kabla ya juzi kati kuibua suala la majeruhi ya Shomari Kapombe basi ni shida tupu.

Tuyaache hayo ya Ndimbo, ndio utamu wa soka letu kubwa ni jinsi Simba ilivyoweza kubutua kombolela na kuipa nafasi Tanzania kuwa na timu nne kwa mara ya kwanza katika mashindano ya klabu Afrika.

Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitapigia saluti Simba kwa walichokifanya msimu huu Ligi ya Mabingwa hadi kufika hatua ya robo fainali ni mfano wa kuigwa kwa timu zetu.

Kikubwa baada ya kombolela kubutuliwa ni vyema klabu zetu Simba, Yanga, Azam, KMC kutambua Agosti 9-11 mashindano hayo yanaanza kinachotakiwa ni kufanya usajili.

Taswira inawataka viongozi wa klabu hizi kuhakikisha mechi za nyumbani zinatumika vizuri kwa kushinda kama ile kauli mbiu ya Simba kila mtu ashinde kwao lakini mwaka huu tunaongeza ugenini tunataka sare.

Hii ni nafasi kubwa kwa klabu zetu ni lazima kuwa na bajeti ya kutosha ya maandalizi ndani na nje ya uwanjani bila.

Naamini KMC taarifa hizi kwao zitakuwa ni nzito, lakini wanachotakiwa kufanya ni kujipanga na kuamua hakuna litakaloshindikana.

Azam wanapaswa kufanya Azam Complex kuwa machinjioni kweli hakuna timu kuchukua pointi kirahisi Chamazi kwa kucheza mpira ndani ya uwanja.

Mashabiki wa Simba na Yanga naamini utani wa jadi utakolea zaidi na kuongeza hamasa ya michezo hii ya Ligi ya Mabingwa kwa sababu kombolela limebutuliwa tusizubae na kurudi nyuma.

Kufuzu hatua ya makundi ni kujihakikishia kupata fedha nyingi kwa klabu hususika, pamoja na kuhakikishia Tanzania kuendelea kuwa na timu nne katika mashindano hayo. Simba imebutua kombolela, Yanga, Azam, KMC kajificheni mkomboe soka la Tanzania.

Advertisement