Simba iliwezwa hapa na Prisons

Muktasari:

Wachezaji wa Prisons, wamefichua siri iliyo nyuma ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba, kwamba waliingia uwanjani wakiwa na mambo mawili, yaliowaaminisha watashinda na wakafanikiwa katika hilo.

WACHEZAJI  wa  Tanzania Prisons,  Lambert Sabiyanka (straika) na Salum Kimenya (kiungo), wamefichua siri ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba, kwamba imetokana na kujua ubora na mapungufu ya wapinzani wao.

 

Wameliambia Mwanaspoti jana Alhamisi ya oktoba 22, mwaka 2020 mara baada tu ya kumaliza mechi hiyo, iliyopigwa Uwanja wa Nelson Mandela, uliopo mkoani Rukwa, kwamba baada ya kujua mambo hayo mawili, walicheza kwa nidhamu kubwa.

 

Sabiyanka amesema licha ya kuwafunga, Simba sio timu ya kuibeza, amefafanua ina wachezaji makini na kwamba hilo walilijua mapema ndio maana waliamua kuwaheshimu na kujua ni namna gani wanaweza wakapata matokeo mazuri.

 

"Tumeifunga Simba kwa sababu tulipata muda wa kuwasoma vyema, aina ya uchezaji wao, hivyo tukawa na nidhamu, huku umakini wa kutumia nafasi za kufunga ukiwa mkubwa, ndio maana ilipopatikana tukafunga na dakika 90 ziliamua sisi ndio wababe kwa mchezo huo,"amesema Sabiyanka na ameongeza kuwa,

 

"Yote kwa yote Simba ina kikosi kizuri, ingawa kwenye mchezo wetu bahati ilikuwa yetu, hivyo watakaocheza nao kwenye mechi zinazoendelea wasiwapuze kwani wanaweza wakachezea kichapo cha maana,"amesema.

 

Kwa upande wa Kimenya,  amesema walitumia vyema dakika 90 ambazo ziliamua wao watoke kifua mbele, ingawa amekiri Simba ilionyesha ushindani wa hali ya juu katika mechi hiyo.

 

"Tuliiheshimu Simba ndio maana tumepata matokeo, lakini tungeingia kwa kujiachia sana, bila shaka tungekuwa na wakati mgumu wa sisi kupata matokeo kwasababu ina kikosi bora na kinachojua kushindana.

 

"Lakini kwa sasa tunaachana na hayo, tunaangalia nini kipo mbele yetu ili tuweze kuangalia ni namna gani tunahitaji pointi zaidi na sio kuifunga Simba iwe mwisho wetu, bado tuna safari ndefu,"amesema Kimenya.