Simba ilipokamilisha siku 137 za jasho na damu Ligi ya Mabingwa Afrika

Monday April 15 2019

 

Dar es Salaam.Mabingwa wa soka Tanzania Simba, imemaliza kazi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni historia ya klabu hiyo kwa michuano hiyo mikubwa ngazi ya klabu Afrika.

Simba imetolewa na TP Mazembe kwenye hatua ya mtoano wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa mabao 4-1, ikiwa ni jumla, baada ya kutoka suluhu mchezo wa kwanza uliofanyika siku 10 zilizopita, Dar es Salaam.

Mabingwa hao wa soka Tanzania wamehitimisha safari yao baada ya siku 137, walianza Novemba 28 mwaka jana ikicheza na Mbabane Swallows na kuwazabua mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya kuwatandoka mabao 4-0 kule kwao eSwatini.

Baada ya hapo, Simba ilicheza na Nkana Red Devils, walifungwa mabao 2-1 lakini marudiano wakashinda mabao 3-1 na kufuzu hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 4-3.

SIMBA YAONGOZA TIMU KUTOKA

Simba na timu nyingine tatu, zimeaga michuano hiyo hatua ya robo fainali. TP Mazembe iliifunga Simba mabao 4-1 lakini pia miamba mingine ya Costantine ya Algeria imepigwa mabao 6-3, Horoya (Guinea) 5-0 na Al Ahly ya Misri imetolewa na Mamelodi kwa kuchapwa mabao 5-1.

Kuingia nusu fainali, TP Mazembe inaungana na Mamelod (Afrika Kusini), Waydad Casablanca (Morocco) na Esperance ya Tunisia.

 MAKUNDI

Simba ilipangwa Kundi D la michuano hiyo ikiwa miongoni mwa timu 16 Bora Afrika, ikiwa pamoja na Al Ahly ya Misri, JS Saoura (Algeria) na AS Vita ya DR Congo.

Ilianza kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JSS mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, kabla ya kutoka na kufungwa 5-0 na Al Ahly na baadaye AS Vita kwa idadi hiyo.

Salama ya Simba hadi kuvuka ilitumia uwanja wa nyumbani vizuri, iliifunga Al Ahly bao 1-0 lakini pia ikaifunga AS Vita. Simba ni wepesi zaidi kwa mechi za ugenini ukiacha ile ya Mbabane, kwani ilifungwa mabao 2-0 na JS Saoura.

Kutoka Kundi D, Simba ilifuzu baada ya kukusanya pointi tisa kwa kushinda mechi tatu za nyumbani. Ilipangwa na TP Mazembe na ilitoka nayo suluhu mchezo wa kwanza kabla ya kukamilisha siku ya 137 kwa kufungwa mabao 4-1.

Simba inarudi nyumbani kucheza Ligi Kuu ikimalizia viporo vyake, huku ikivuna Dola650,000 pia imekata tiketi ya kucheza raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa endapo itatwaa ubingwa Bara na kucheza tena ligi hiyo inayoanza baadaye Agosti mwaka huu.

SOMO LA SIMBA

Simba imetoa somo la aina yake kwa wawakilishi wengine wa klabu huku ikitimiza malengo yake ya kuingia hatua ya makundi. Kwa bahati nzuri kwenye makundi wakafuzu. Kuna mambo kadhaa nayaona hapa.

Kwanza; Malengo yao kwa msimu huu yamekamilika kwa asilimia 100 kwa kuwa mipango ya awali ni kuingia makundi na wamefanikiwa na robo fainali ilikuwa ziada na juu ya hapo, ingekuwa ziada zaidi.

Mpango wa klabu na kocha wake, Patrick Aussems ni kuivusha Simba hatua ya makundi, mpango ambao ameutimiza na kufika robo fainali.

Pili; Somo kubwa la kujifunza, uwanja wa nyumbani hufanyiwi makossa. Simba ilitumia kikamilifu kwa kushiunda mechi zote tano ukiacha moja ya TP Mazembe waliyotoka suluhu. Kama ilivyokuwa TP Mazembe, imeshinda mechi zote nyumbani.

Simba imejitangaza vya kutosha, hakuna timu inayoweza tena kufurahia kukutana na Simba endapo itatwaa ubingwa wa Ligi Kuu na kurudi Ligi ya Mabingwa. Leo hii hata TP Mazembe, Al Ahly, AS Vita watakuwa wanajiuliza na kuja kwa wasiwasi wakisikia Simba.

NJE YA TANZANIA

Kati ya vitu ambavyo Simba imeonyesha udhaifu ni kushindwa kupata ushindi nje ya uwanja wake wa nyumbani, ukiachilia mbali mchezo wa kwanza wa hatua ya awali dhidi ya Mbabane Swallows.

Simba imepoteza mechi zake zote ilizocheza nje huku ikiruhusu mabao mengi zaidi na licha ya nyumbani kushinda, lakini kwa kiasi kidogo.

Nje ya Uwanja wa Taifa, Simba imefungwa mechi zote ikiruhusu mabao 18 na yenyewe ikifunga mabao sita. Ilishinda 4-0 na Mbabane, ikafungwa 2-1 na Nkana na 4-1 la TP Mazembe. Uwanja wa nyumbani imefunga mabao 13 na imefungwa mabao matatu.

Kuna kila sababu ya kufanyia tathmini eneo hili la mechi za ugenini. Simba inapotea inapokuwa ugenini kwa mechi zote, hatua ambayo ni rahisi kuitoa.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba, inafungwa mabao mengi, ambayo hata yenyewe haijawahi kutoa kipigo kikali zaidi ya kuilaza JS Saoura ambao hata hivyo hawakuwa na ubora na uzoefu wa michuano ya klabu Afrika.

USAJILI

Simba, Yanga na timu nyingine zimechelewa kwa kukimbilia kunyang’anyana wachezaji. Baadhi ya wachezaji hawa hawa wanaowagombania kila msimu wa usajili, baadhi hawana tija wala ubavu wa kukutana na miamba ya soka Afrika.

Mfano, Simba ingekuwa na wachezaji legelege wasingefika mbali. Mechi ya Nkana Red Devils ilikuwa ya mapambano hasa sanjari na ile ya AS Vita. Wachezaji walitunisha msuli wa mapambano ambayo mwisho wa siku yalijibu.

Fomu kwa mchezaji ni kitu muhimu. Mchezaji anatakiwa kuwa kwenye ubora wake mwanzo mwisho. Nidhamu ya uchezaji haizingatiwi kwa wachezaji wetu ndio maana leo wanaonekana bora kesho kiwango kiko chini. Mfano mzuri ni Lionel Messi, kila siku yeye ni mpya.

Timu zitakazofuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa, Kombe la Shirikisho lazima kufanya usajili makini wa wachezaji wenye ubora wa kuhimili mikikimikiki ya mashindano hayo makubwa kwa klabu Afrika.

Klabu zinazoamini kuwa zina nafasi ya kutwaa ubingwa wa FA au Ligi Kuu, ni wakati wa kupeleka maskauti kila mahali kusajili wachezaji ambao wapo tayari, soka yao inaonekana kutoka katika klabu kubwa. Ubora wa wachezaji wanaonekana kwenye klabu zao, lakini si wachezaji wanaochukuliwa kimyakimya na wakija hapa wanakaa benchi.

Wachezaji kama Makusu, Ngoma, Mundele ni kati ya wachezaji wanaotisha. Mpira ni gharama na kuwachomoa na kuwaleta ni gharama na mafanikio hayaji kama gharama hazitumiki.

Klabu zenye nafasi, eneo zuri la kupata wachezaji makini ni hapa ambako timu zimefuzu nusu fainali.

LIGI YA USHINDANI

Klabu kusajili wachezaji wakali, kutasababisha ushindani mkali kwenye Ligi Kuu Bara. Ushindani wa wachezaji utaongeza msisimko lakini pia kutengeneza mazingira ya ushindani bora kwenye timu ya taifa.

Siku zote ligi legelege huzaa timu ya taifa legelege, kwa hiyo timu ya taifa hutegemeana na ubora wa wachezaji.

Advertisement